Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
ALIYEWAHI kuwa mlinzi wa Rais wa zamani wa Gabon, Omar Bongo, Jin
Yung Kim, ameanza kuwanoa walimu wa mchezo wa taekwondo mjini Arusha
katika mafunzo yaliyoanza juzi.
Awali Shirikisho la Taekwondo (TTF), lilitegemea washiriki 30 kutoka
mikoa ya Kilimanjaro, Simiyu, Kagera, Mwanza, Dar es Salaam, Arusha
pamoja na Serengeti, lakini hadi mafunzo hayo yanafunguliwa, washiriki
walikuwa ni 17 tu, hivyo 13 walikuwa bado kuripoti.
Mafunzo hayo ya siku 12 yaliyozinduliwa na Katibu Mkuu wa Kamati ya
Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi, ni sehemu ya mikakati ya kuleta
mageuzi ya mchezo huo nchini.
Mafunzo hayo yataendeshwa na mtaalamu wa Shirikisho la Taekwendo la
Dunia (WTF), kutoka Korea ya Kusini, Jin-Yung Kim na kuratibiwa kwa
upande wa utawala na Samwel Mwera wa TOC na Makamu Mwenyekiti wa TTF,
Joseph Chuwa kwa upande wa ufundi.
Akizindua mafunzo hayo, Bayi aliupongeza uongozi wa TTF kwa
kufanikisha mafunzo hayo sio tu kuanza kwa muda uliopangwa, pia kwa
ushirikiano na WTF, kumpata mkufunzi kijana na mahiri kutoka Korea ya
Kusini, Jin Yung Kim.
“Nimefahamishwa, Kim ni mtaalamu, mpiganaji na mkufunzi mzuri vile
vile kwa kutambua vipaji vya wachezaji wa mchezo wa taekwondo.
“Umahiri wake huo, ndio uliomfanya wakati fulani hapo nyuma kuwa
mlinzi wa Rais wa Gabon, marehemu Omar Bongo. Ni matumaini yangu
mtafaidika na mafunzo yake,” alisema Bayi.
Alisema mara ya mwisho anakumbuka mafunzo kama hayo yalifanyika
jijini hapa mwaka 2006, kwa WTF kumleta mkufunzi Sang Min– Baik kutoka
Korea ya Kusini.
“Ndugu Makamu Mwenyekiti (Chuwa), mafunzo haya ni ya gharama
yanayogharimiwa na Olimpiki Solidarity kupitia Kamati ya Olimpiki
Tanzania, nashauri washiriki watakapomaliza mafunzo haya, wawe na chachu
ya kuuendeleza mchezo wa taekwondo katika maeneo na mikoa yao
wanayotoka,” alisisitiza Bayi.
Aliwaomba TTF kuweka jitihada kubwa katika kuwekeza kwenye shule kwa
vijana wadogo, ambao ni rahisi zaidi kuwafundisha kwa kuwa na unyumbufu
mkubwa.
Aliwaomba TTF kuandaa mashindano ya mara kwa mara ya taekwondo kwa
ngazi mbalimbali, hasa kuhusisha klabu au mashirikisho ya mikoa kama
yapo, kwani bila kufanya hivyo, uongozi hauwezi kutambua matunda ya
walimu hao wanaonolewa.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment