Home » » WANANCHI KUNUFAIKA MRADI WA MABADILIKO TABIA NCHI

WANANCHI KUNUFAIKA MRADI WA MABADILIKO TABIA NCHI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

ZAIDI ya wakulima na wafugaji 150,000 kutoka katika wilaya ya Monduli Mkoa wa Arusha wanatarajia kunufaika na mradi wa mabadiliko ya tabia nchi.

Mradi huo utagharimu kiasi cha sh.bilioni 3.5 na utaweza kusaidia wilaya hiyo kuondokana na ukame ambao umesababishwa na mabadiliko hayo.

Hata hivyo mradi huo utaanza kutekelezeka kuanzia mwezi Oktoba mwaka huu, ambapo utatekelezwa katika wilaya tatu ikiwemo Longido, Monduli na Ngorongoro zikishirikiana na Shirika la IID /Haki kazi catalyst pamoja na serikali ya Uingereza kupitia shirika lake la U.K.A.D.

Akiwasilisha taarifa hiyo katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo mchumi na mratibu wa mradi wa mabadiliko ya hali ya hewa ya nchi wilayani humo, Joseph Ruta alisema kuwepo kwa wazo la mradi huo kulitokana na athari za ukame zilizotokea 2008-2009.

Alieleza kuwa kutokana na athari hizo viongozi pamoja na wabunge walishauriana jinsi ya kuwa na mradi, ambao utawawezesha wananchi kukabiliana na athari za mabadiliko ambayo yamekuwa yakileta hasara kwa jamii.

Ruta alidai kuwa kupitia mradi huo ambao unatarajiwa kuanza hivi karibuni utasaidia kwa kiwango kikubwa sana kuwajengea wakulima na wafugaji uwezo wa kukabiliana na mabadiliko hayo pindi yanapotokea na kuwafanya wasiathirike nayo.

“Mradi huu tunatarajia utatekelezwa kuanzia Oktoba na utaweza kuwajengea wananchi uwezo mkubwa, kwani hata kama mabadiliko ya hali ya hewa yatatokea bado wakulima wataweza kwa namna gani wakabiliane nayo ili kuhakikisha shughuli zao zinazidi kusonga mbele,”aliongeza.

Aliongeza kuwa watu zaidi ya laki moja wataweza kunufaika na mradi huo kwa kuwa vijiji vyote vilivyopo katika tarafa za Kisongo, Manyara na Makuyuni wataweza kunufaika na mradi huo ambao utaweza kuchukua muda wa miaka 4.

Aidha mratibu huyo aliwataka viongozi, wataalamu pamoja na wananchi kutoa ushirikiano zaidi ili kuwezesha mradi huo usonge mbele zaidi kwa kuwa kufanikiwa kwake kunahitaji nguvu kuunganishwa kwa pamoja.

chanzo;Majira

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa