Home » » VIONGOZI WA SOKA ARUSHA WAMRUKA DC ARUMERU

VIONGOZI WA SOKA ARUSHA WAMRUKA DC ARUMERU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
SAKATA la vijana wa The Dream Team ya Arumeru mkoani hapa kutelekezwa nchini Brazil, limechukua sura nyingine baada ya Chama cha Soka Mkoa (ARFA), kuruka kimanga kujihusisha na uratibu wa safari hiyo.
Hivi karibuni iliripotiwa vijana hao kutelekezwa nchini Brazil na Mkuu wa Wilaya (DC) ya Arumeru, Nyirembe Munassa Sabi, ambaye inaelezwa ndiye aliyesimamia mpango huo, ikiwamo kuchangisha fedha kwa wadau mbalimbali.
Mwakilishi wa Klabu Mkoa, Omary Walii, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), alisema jijini hapa jana kwamba hakuhusishwa na jambo lolote la safari ya vijana hao kwenda Brazil, ingawa alisikia juu juu kutoka kwa wadau wa soka.
“Mimi nilisikia tu kwamba kuna vijana walioundwa na DC na wanajiita The Dream Team na wanatarajia kwenda Brazil, lakini sikuhusishwa na jambo lolote la kuwaratibu vijana hao, kwani nilipochunguza zaidi na kugundua ni mkuu wa wilaya anahusika, nilipata hofu masuala haya ya soka yanaweza kuingiliana na siasa, hivyo ndiyo nikajitoa kabisa,” alisema na kuongeza:
“Na hata siku waliyoondoka sijui, bali nimekuja tu kusikia kuwa vijana wameondoka na sijui hata idadi yake, hivyo kama anasema TFF wanahusika labda niulize makao makuu Dar es Salaam juu ya hili, ila uliza chama cha soka mkoa wanaweza kujua hili.”
Katibu Mkuu wa ARFA, Adam Brown, alisema kuwa mwanzo wa mchakato kuna barua ilipelekwa ofisini kwake kutaarifu kuwa kuna vijana wanafanyiwa mpango wa kwenda kushuhudia michuano wa Kombe la Dunia nchini Brazil.
“Baada ya kuletewa barua hiyo, Mkuu wa Wilaya alikuja kunitaka nimsaidie kwenda ofisi za Uhamiaji kurahisisha vijana hao kupata pasipoti, ambapo aliniletea majina zaidi ya 30.
“Mimi niliamua kufanya hilo, lakini unaambiwa tangu vijana hao wafanikiwe kupata pasipoti sikujua tena kilichoendelea, wala kuhusishwa tena kwa lolote na mimi sikufuatilia tena, bali nilipata taarifa tu juu juu kutoka kwa watu kuwa vijana wameshaondoka kwenda Brazil, lakini sijui ni wangapi hadi leo,” alisema Brown.
Alipotafutwa DC Nyirembe kuweka sawa tuhuma hizo, aligeuka mbogo huku akitishia kuishitaki ARFA kwa kukana kuhusika hilo, sambamba na mwandishi wa habari hizi.
“Wewe si ndio Bertha uliyeniandika vibaya kwa kuhongwa na watu waliochukia vijana hawa kwenda Brazil, sasa usiniulize chochote na wala sina jibu lolote… mimi nawafahamu sana waandishi wa habari, na mimi namiliki chombo cha habari cha redio, hivyo hakuna nisichokijua na nikitaka leo au kesho nakufungulia mashitaka wewe na hao viongozi wa mpira, kwani nina mawakili wa kutosha,” alisema.
Aliongeza kuwa yeye ni mpenzi mkubwa wa soka na lengo lake la kuanzisha timu hiyo na kuwapeleka Brazil kushuhudia Kombe la Dunia ni kuwafanikisha vijana hao kuona na kujua mbinu mbalimbali za soka, ili kuzitumia na kusakata soka vema na baadaye kufanikiwa kucheza Kombe la Dunia mwaka 2025 na kuipeperusha bendera ya Tanzania.
“Mimi nina malengo makubwa sana na hii timu, ikiwemo kucheza Kombe la Dunia mwaka 2025, lakini nashangaa watu wananipiga vita mimi badala ya kupiga vita uzembe wao wafanikiwe hata kupata timu itakayowakilisha Arusha Ligi Kuu,” alisema.
Alieleza kuwa vijana hao si kweli walitelekezwa, bali alikuwa nao katika hoteli ya Mega Pool iliyoko Brazil hadi waliporejea nchini.
Awali vijana sita walifanikiwa kupata nafasi ya kwenda Brazil kwa michango ya wahisani chini ya DC, lakini baadaye taarifa zilifika nchini kuwa vijana hao wamekosa makazi kwa siku kadhaa na kulazimika kulala uwanja wa ndege na stendi ya mabasi  huku mkuu huyo wa wilaya akikataa kuzungumzia chochote, kwa madai kuwa suala hilo liko mikononi mwa TFF
 Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa