Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MFANYAKAZI wa Kampuni ya simu ya Tigo, (MIC T Ltd.), jijini hapa,
Mwita Makore, amekutwa amekufa nyumbani kwake maeneo ya Kimandolu huku
akiwa na kamba za viatu shingoni kuashiria kwamba alijinyonga nazo kwa
kujitundika kwenye bomba la bafuni kwake.
Hali hiyo imezua gumzo miongoni mwa wakazi wa jiji hili wakihoji
inawezekanaje mtu kujinyonga kwa kamba ya viatu hadi kufa huku wengine
wakihoji uwezekano wa mwili wa mtu mzima kuning’inia kwenye bomba la
bafuni.
Habari kutoka eneo la tukio zinadai kuwa mwili wa Makore ambaye
alikuwa kitengo cha ‘store’, ulibainika Juni 20, mwaka huu baada ya
kutoonekana wala kupatikana kwa simu zake za kiganjani kwa siku mbili
mfululizo, hali iliyowalazimu wafanyakazi wenzake kwenda kumtafuta
nyumbani kwake na kubaini kifo chake.
Mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo jijini hapa aliyezungumza kwa
sharti la kutotajwa jina lake, alisema mara ya mwisho Makore kuingia
ofisini ilikuwa ni Juni 18, mwaka huu.
“Unajua yeye kazi yake haimlazimu kuwa ofisini muda wote, hivyo
akishamalizana na wateja wake huondoka, hivyo siku ya Alhamisi hakuja
kabisa ofisini, lakini hakuna aliyekuwa na wazo kama kakutwa na jambo
baya.
“Alikuja mteja anayehitaji vocha, ikabidi apigiwe simu, simu ikawa
inaita haipokelewi, siku inayofuata wakaja wateja wengine, Mwita
akapigiwa simu zake zikawa zinaita tu lakini hazipokelewi.
“Yule mteja akachukia akaamua kupiga simu makao makuu kueleza
usumbufu anaoupata, ndipo nao wakawapigia viongozi hapa wakawaeleza
kama hapokei simu kwanini wasimfuatilie nyumbani kwake pengine amepata
matatizo,” alisema mfanyakazi huyo.
Alisema kuwa walipofika nyumbani kwake walikuta gari ya Kampuni ya
Tigo ikiwa imeegeshwa vizuri, lakini funguo zake ziko ndani na milango
imerejeshewa tu huku kwenye mlango wa kuingia ndani kwa Makore kukiwa na
viatu vyake na walipopiga simu zake, wakasikia zikiita kutoka ndani
ndipo wakaamua kuingia ndani.
“Tulipoingia pale mezani tulikuta kuna chupa ya soda, na simu zake
tatu pamoja na kadi zake za benki, tukaendelea kuangalia maeneo
mbalimbali ya nyumba hiyo ndipo tukamkuta Makore bafuni na kamba ya
viatu shingoni,” alisema mfanyakazi huyo wa Tigo.
Mwananchi mwingine anayeishi maeneo ya Kimandolu, alisema tukio hilo
limewashangaza sana kwani Makore alikuwa kijana mtaratibu asiye na
makuu na alikuwa mpenzi wa mchezo wa pool table.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas, alithibitisha kutokea
kwa kifo hicho alichodai ni cha kawaida kwani amekutwa amekufa nyumbani
kwake na hakuna mahali palipovunjwa.
“Achana na habari za barabarani, amekutwa amekufa nyumbani kwake,
hakuna mahali pamevunjwa, hiyo ni ‘natural death’,” alisema Sabas
wakati Tanzania Daima ilipokuwa ikimweleza kile kinachoelezwa na
majirani pamoja na wafanyakazi wenzake.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment