Home » » WATUHUMIWA ULIPUAJI BOMU ARUSHA WABURUZWA KORTINI

WATUHUMIWA ULIPUAJI BOMU ARUSHA WABURUZWA KORTINI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Watuhumiwa 16 wa shambulizi la bomu kwenye baa ya Arusha Night Park wafikishwa mahakamani.
Watuhumiwa  16 wa shambulizi la bomu kwenye baa ya Arusha Night Park, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, huku ulinzi ukiimarishwa kwenye eneo hilo.
Wanashitakiwa kwa makosa 16 ya kuua, kujaribu kuua na kushawishi vijana kujiunga na kusaidia kikundi cha kigaidi cha Al Shaabab.

Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakiwa kwenye magari na polisi walitanda mahakamani hapo kuanzia asubuhi.

Miongoni mwa akari hao walikuwa wamevaa sare na wengine wakiwa kwenye mavazi ya kiraia.

Mwendesha Mashataka Wakili wa Serikali, Khalili Muda, aliwasomea mashtaka tisa ya kuua kinyume cha kifungu cha 196 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Watuhumiwa hao wanadaiwa kumuua Sudi Ramadhan ambaye alifariki  dunia akiwa anapata matibabu hospitali ya mkoa wa Arusha ya Mount Meru, Mei 13 mwaka huu.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Abdallah Athumani Labia (34) mkulima na mkazi wa Mang’ola wilayani Karatu, Abdulkarim Thabit Hasia (32) mkazi wa Ngusero, Hassan Zuberi Saidi (28) mkazi wa Tengeru na  Rajab Phiri Hemedi (28) mkazi wa Magugu Babati.

Wengine ni Ally Hamisi Kidaanya (32) mkazi wa Magugu-Babati, Abdallah Maginga Wambura (40) mkazi wa Kwa Mromboo-Murriet, Shabani Abdallah Wawa (22) mkazi wa Magugu-Babati, Ally Hamisi Jumanne (25) mkazi wa Matufa-Babati na Yassin Hashim Sanga (26) mkazi wa Kahama.

Aidha Wakili Muda alidai mahakamani hapo kuwa watuhumiwa hao walijaribu kuwaua watu 14 katika tukio hilo, kinyume cha kifungu cha 211 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Aliwataja waliojeruhiwa ambao wote ni wakazi wa Arusha kuwa ni Joyce William (38), mtaa wa Moshono, Evance Maleko (26) Sanawari, Loyce John (29) Sanawari, Evarist Richard (34) Kijenge, Petro Bakenege (25) Mianzini, Msafiri Mushi (28) Sombetini na Pius Shayo (51) Kaloleni.

Wengine ni Antelus Ishengoma mkazi wa Mianzini, Sudi Ramadhani (38) Mianzini, Mariam Hans (26) Mianzini, Nathani Charles (28) Mianzini, Steven Cosmas (25) Mianzini na Gilbert Nkya (36) Moshono.

Hakimu Siyani alisema mahakama yake haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo na akaiahirisha kesi hiyo hadi Juni 12 itakapotajwa tena.

Katika hatua nyingine, mahakama hiyo ililazimika kuhamia kwa muda katika wodi ya hospitali ya Mount Meru, kuwasomea mashataka watuhumiwa wawili ambao hawakuwapo mahakamani.

Aliyesomewa mashtaka yake hospitalini alikuwa Abdallah Maginga Wambura wakati Abdulkarim Thabit Hasia hakuweza kusomewa mashtaka yake kwa kuwa hali yake ni mbaya. Katika shauri la pili, Wakili wa Serikali Marcelino Mwamunyange, watuhumiwa wanane walisomewa shtaka moja la kushawishi na kuhamasisha watu kujiunga na kikundi cha kigaidi cha Al Shabab.

Alisema kati  ya 2010 hadi Februari mwaka huu maeneo mbalimbali nchini watuhumwa Swalehe Hamisi (51) mkazi wa Sombetini, Abdallah Yassin (33) mkazi wa Tunduru na Sudi Nasibu Lusuma (18) mkazi wa Mwanza waliwashawishi watu wajiunge na kusaidia kundi la kigaidi la Al Shabab.

Hakimu Siyani alisema kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza shauri hilo, aliliahirisha hadi Juni 11, mwaka huu itakapotajwa tena. Watuhumiwa wote wapo rumande.
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa