Home » » KAIJAGE AKUNWA NA VIPAJI ARUSHA

KAIJAGE AKUNWA NA VIPAJI ARUSHA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
KOCHA wa timu ya taifa ya soka ya wanawake, Twiga Stars, Rogasian Kaijage, amefurahishwa na kiwango cha kusakata soka kwa timu za wanawake za Mkoa wa Arusha.
Mbali na kuwapongeza, Kaijage aliahidi kuwatumia wachezaji nyota kutoka katika timu hizo na kuunda timu mpya ya taifa.
Kaijage aliyasema hayo jijini hapa hivi karibuni, baada ya kufanyika bonanza la wanawake la timu za Mkoa wa Arusha za vijana wenye miaka chini ya 18 ambapo ilishuhudiwa Testimony ikiibuka mshindi ikifuatiwa na St. Jude na mwisho timu ya Future Star.
Kaijage alisema kuwa awali alidhani timu za mpira wa miguu ziko Dar es Salaam na Mwanza pekee, lakini sasa amegundua hata Arusha pia zipo, hivyo kinachofuata sasa ni kuunda timu mpya ya taifa kwa kutumia nyota kutoka timu za mikoani.
“Awali tulikuwa tunaangalia Mkoa wa Dar es Salaam pekee kwa upande wa soka la wanawake na hivi karibuni pia nimeona viwango vya Mkoa wa Mwanza, lakini sasa pia nimeona Arusha kuna timu za wanawake, wanajua kusakata soka kuliko hata mikoa mingine mbali na kukumbwa na changamoto nyingi, ambazo hata hivyo zinatatulika,” alisema.
Aliwaasa wachezaji hao kuendelea kujifua kimazoezi na kujiweka vizuri zaidi, ili siku mtu akipata nafasi ya kuja kwenda kuonyesha uwezo wake, ionekane kweli anafaa kuitwa kwenye timu ya taifa.
Kutokana na baadhi ya wachezaji waliokuwa wakiumia na kukosa huduma ya kwanza, Kaijage alisema kuwa ameona changamoto wanazokumbana nazo na kuwataka wamiliki wa timu hizo na wakuu wa shule husika, kuhakikisha zinatatuliwa kwa kila timu kuwa na madaktari wake au kuwa na daktari mmoja wa kuhudumia timu zote zinapokuwa uwanjani.
Bonanza hilo lililoandaliwa na taasisi ya Testimony, lilikuwa na kaulimbiu isemayo; ‘Michezo ni Furaha, Afya na Ajira’
.Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa