VIJANA
zaidi ya 1,000 ambao ni wanachama wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha
Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Meru, Mkoa wa Arusha, wamevamia ofisi za
chama hicho kuanzia ngazi ya wilaya na mkoa, wakidai wamechoshwa na
uongozi wa juu wa chama kuwachagulia viongozi ambao si chaguo lao.
Vijana
hao walidai viongozi waliopo makao makuu ya chama hicho wamewaonea kwa
kutangaza uamuzi wao wa kuwachagulia viongozi tofauti na matakwa yao.
Alisema wao walimchagua Kamanda wao, John Palangyo, lakini uongozi wa CCM makao makuu walitofautiana nao.
Maandamano
hayo ambayo yaliratibiwa na wajumbe wa UVCCM Meru, yalisababisha
shughuli mbalimbali za chama hicho kuanzia ofisi ya wilaya hadi mkoa
kusimama kutokana na baadhi ya vijana hao kulazimika kuingia kwa nguvu
ndani ya ofisi hizo, kisha kushinikiza kusikilizwa kwa madai yao.
Akizungumza
kwa niaba ya wajumbe hao mmoja wa wajumbe hao, Joshua Mbwana, alisema
kilichosababisha wafanye maandamano hayo ambayo yalianzia Usa River
Arusha ni kuelezea umma kuwa wapo baadhi ya viongozi katika chama hicho
ambao wanawachagulia viongozi wa kuwaongoza bila kuwauliza.
“Hivi
juzi tulimchagua kamanda wetu ambaye ni John Palangyo na tulimpitisha,
lakini baada ya jina kufika mkoani ghafla jina lilibadilishwa kama
haitoshi makao makuu wakasema kuwa wana mtu wao... sasa je, wao ndio
wanatuchagulia mtu wa kutuongoza au sisi? Kamwe hatutakubali na badala
yake tutapigana hadi mwisho hii tabia imetuchosha sana,” alisisitiza
Joshua.
Alidai endapo hali hiyo itaendelea kufanyika mapambano yatakuwa makubwa sana.
Alisema
pamoja na kuwa wamevamia ofisi za CCM; kama hawatapewa majibu ya
kuridhisha ndani ya siku nne kuanzia sasa huenda wakaandamana hadi makao
makuu ya ofisi za CCM.
“Tumesharatibu maandamano hayo, maandalizi
yanaenda vizuri itakuwa ni historia kwa CCM kutuchagulia viongozi kwa
masilahi yao binafsi na matakwa ya viongozi wa ngazi za juu hasa wale
ambao wana malengo ya kugombea nafasi za ubunge katika majimbo yao,”
alisema na kuongeza;
“Ujumbe wetu ni lazima tutauweka wazi na kila
mtu aweze kusoma, lakini hata kuingia ndani ya ofisi hizo bila taarifa
wala kibali cha aina yoyote ile,” alisema.
Katibu wa CCM Wilaya ya
Meru, Langaeli Akyoo, alisema kuwa mchakato wa kumpata kiongozi ambaye
vijana hao wanamtaka ulienda vizuri na majina matatu yalifikishwa Dar es
Saalam makao makuu ya chama, lakini baadaye hayakurudi kama
ilivyotarajiwa.
Akyoo alisema majina mawili yalirudi, lakini majina
mawili ambayo yana utata mkubwa ndiyo yalisababisha maandamano makubwa
kuanzia Meru hadi Arusha.
“Jamani maombi yenu nimeyapata na
ninapenda kuwaambia kuwa majina ambayo yalienda Dar es Salaam makao
makuu yalirudishwa mawili ambayo yana utata na wao walisema kuwa
mchakato unatakiwa kuanza moja jambo ambalo sisi hatukubaliani nalo
kabisa,” alisema Akyoo.
Awali, mwenyekiti wa umoja wa vijana wilaya
hiyo, Bw Elirehema Mbisse alisema kuwa, mchakato wa kumpata Kamanda huyo
unaendelea na hivyo amewataka wawe na subira ili waweze kuangalia namna
ya kutatua tatizo hilo ambalo limesababisha ofisi za CCM kusimamisha
kazi kwa muda.
Uongozi wa UVCCM kupitia kikao chake cha kamati ya
utekelezaji kilipendekeza majina matatu ambayo ni John Palangyo, Sioi
Sumari na Daniel Palangyo.
Baada ya miniti kupelekwa mkoani ambapo
mkoa ulijiridhisha na majina hayo na uliweza kuhoji na hatimaye waliweza
kumpata John Palangyo kama Kamanda wa Vijana Wilaya ya Meru,lakini
baadaye barua ilikuja na kudai kuwa kamanda wa Meru si huyo jambo ambalo
si la kweli.
Chanzo:Majira
0 comments:
Post a Comment