Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
HATUA ya Jeshi la Polisi kuzuia mikutano ya wabunge wa upinzani
majimboni kwao kwa kisingizio kwamba inagongana na ile ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM), imemwibua Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema
(CHADEMA) na kumtaka mkuu wa polisi wilayani hapa (OCD), Gires Muroto
kuacha kufanya kazi kwa maelekezo ya kisiasa badala yake asimamie
sheria na kanuni.
Lema alisema hatua ya OCD huyo kufuta mikutano yake ya kibunge
aliyokuwa ameiruhusu kwa kigezo kuwa amepokea maombi mengine ya CCM ya
kufanya mikutano kwenye maeneo aliyokuwa amemruhusu kufanya mikutano ni
ya ubabaishaji.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano, Lema alisema kuwa Aprili 17,
mwaka huu, alimwandikia barua OCD akiomba kufanya mikutano ya wananchi
kwa nafasi yake kama mbunge kwenye kata za Levelosi, Terrat, Daraja
Mbili na Moshono kwa tarehe tofauti.
Alisema kuwa siku hiyo hiyo alipokea barua toka kwa OCD akimruhusu
kuendelea na mikutano yake, lakini katika hali isiyo ya kawaida, Aprili
20 akapokea barua nyingine kutoka kwa kiongozi huyo akizuia mikutano
hiyo.
“Sababu alizozitoa OCD hazina mashiko, mimi ni mbunge wa wananchi
wote wa Arusha, wakiwemo CHADEMA na CCM, hata Mary Chatanda (Katibu wa
CCM Mkoa) mimi ni mbunge wake, hivyo nilipompa taarifa OCD alipaswa
kuelewa kuwa naenda kuzungumza na wananchi wote wa Arusha, si wa chama
changu pekee, hivyo kuzuia mikutano yangu eti kwa sababu siku mbili
baadaye CCM wameomba kufanya mikutano si sahihi.
“OCD amekuwa akitumia sababu hii kuzuia hata mikutano ya CHADEMA.
Mtakumbuka wakati ule wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Kata ya Sombetini,
maandamano ya CHADEMA kupinga uonevu wa CCM na polisi yalizuiwa kwa
kigezo kuwa CCM nao wanataka kuandamana,” alisema Lema.
Alisema kuwa hoja ya pili aliyotoa OCD kuzuia mikutano yake kuwa
wanazuia mikusanyiko, hasa baada ya bomu lililotokea kwenye baa ya
Arusha Night Park nayo haina ukweli kwani watu wameendelea kukusanyika
maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha ikiwemo baa, sokoni kwenye kumbi za
starehe na zile za ibada.
Katika barua hiyo iliyosainiwa na OCD Muroto yenye kumbukumbu namba
AR/B.5/Vol.III/162 ambayo Tanzania Daima inayo nakala yake, kiongozi
huyo anakiri kupokea barua ya Lema na kuwa alimruhusu kuendelea na
mikutano, lakini anaizuia kwa sababu CCM nao wameomba mikutano maeneo
hayohayo na tarehe hizohizo.
“Itakuwa sio busara kuruhusu mikutano ya hadhara kwa vyama viwili
vinavyopingana kisera, maudhui na mtazamo kufanya mikutano katika
maeneo, muda na siku zinazofanana kwani inaweza kupelekea uvunjifu wa
amani wakati wa mikutano hiyo.
“Hivi karibuni kumetokea tukio la mlipuko wa bomu… tukio hilo
limeleta hofu kwa wananchi na bado limo katika mawazo ya watu,
haitakuwa busara kuendelea kuruhusu mikusanyiko bila kutoa kipaumbele
cha kuimarisha usalama, kwa mantiki hiyo Jeshi la Polisi tumeelekeza
nguvu zetu katika kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yote ya
Jiji la Arusha,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment