Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
SERIKALI
imewataka wenye viwanda nchini kuongeza kasi ya uzalishaji bidhaa ili
kutumia fursa ya soko kubwa la ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na
SADC.
Akizungumza wakati wa hafla ya utoaji tuzo za Shirikisho la
Wenye Viwanda (CTI) mwishoni mwa wiki Waziri wa Viwanda na Biashara,
Abdallah Kigoda alisema hali inavyojionesha sasa inatabiri mwelekeo wa
ushindani mkubwa katika kuendeleza viwanda toka nchi jirani ambazo
zinalenga kutumia fursa za masoko ya ndani na nje ya utaratibu bila
ushuru na bila kikomo (DFQF).
Alisema, Wizara kupitia Mamlaka ya
Maeneo Maalumu ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) inaendelea kutenga
maeneo ya EPZ na SEZ kama moja ya mikakati ya kuvutia uwekezaji na
kuongeza uzalishaji viwandani ili kukuza ajira.
Aliongeza kuwa,
mpaka sasa maeneo haya yametoa ajira kwa wafanyakazi 26,381 hadi kufikia
Juni 2013 na ajira hizo zinatarajia kuongezeka kadri viwanda zaidi
vitapoanza uzalishaji.
Alisema, kuanzia Januari mwaka huu hadi sasa viwanda 13 vimepewa vibali chini ya utaratibu huu.
Vilevile
Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) linaendelea na jitihada za kubuni
na kutekeleza miradi mbalimbali ya kuanzisha viwanda mama ambayo
inatekelezwa kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Mwenyekiti wa (CTI),
Dkt. Samuel Nyantahe aliiomba serikali kuhimiza Mamlaka ya Bandari
(TPA) kuongeza ufanisi wa miundombinu ya Bandari ya Dar es Salaam kwa
kuongeza winchi za kupakulia mizigo bandarini kwani zilizopo
hazitoshelezi.
Pia aliiasa serikali kuharakisha mpango wake wa
kuweka bandari kavu Kisarawe na kuimarisha reli ya kuchukua mizigo
kutoka bandarini ili kupunguza msongamano wa mizigo kukaa bandarini kwa
muda mrefu.
Alisema, hakuna mabehewa na injini za treni za kutosha
hali inayosababisha mizigo mingi mizito kusafirishwa kwa barabara,
usafiri ambao ni wa gharama kubwa na huchangia barabara kuharibika baada
ya muda mfupi.
Aliongeza kuwa, pamoja na matatizo mengi sekta ya
viwanda imefanya vizuri kwa kuongeza mauzo ya bidhaa za viwandani nje ya
nchi.
Alisema mauzo ya nje yaliongezeka kutoka dola za Kimarekani
milioni 861.5 mwaka 2011 na kufikia dola za milioni 1,047.3 mwaka 2012.
Alisema, hilo ni ongezeko la asilimia 21.6.
Mwenyekiti huyo alisema, mauzo ya bidhaa za viwandani yalichangia asilimia 25 ya thamani ya mauzo yote Tanzania nchi za nje.
"Tunategemea
kuwa sekta ya viwanda itaendelea kutoa mchango mkubwa zaidi katika
uchumi wa nchi yetu,ikiwa ni pamoja na kuipatia serikali mapato yake
kutokana na kodi na tozo mbalimbali,"alisisitiza.
Alisema pamoja na
mafanikio hayo katika sekta ya viwanda kwa mwaka 2013 mafanikio hayo ni
madogo ukilinganisha na uwezo na fursa zilizopo.
Dkt.Nyantahe
alisema, katika kusimamia biashara kwenye mfumo wa soko huria, serikali
ilianzisha taasisi za usimamizi na udhibiti wa biashara ili kudhibiti
mwenendo wa kibiashara na kuwalinda walaji.
Alisema taasisi nyingi
zilizoanzishwa zinafanya kazi zinazofanana hivyo kuongeza urasimu na
muda katika utekelezaji wa majukumu yao.
Aidha, taasisi hizo
zimekuwa zikiwatoza wafanyabiashara ada kubwa ili ziweze kugharamia
shughuli zake za kiutendaji hali inayosababisha kuongeza gharama za
kufanya biashara.
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment