Home » » AFC YAANZA SAFARI KUREJEA LIGI KUU

AFC YAANZA SAFARI KUREJEA LIGI KUU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
TIMU ya AFC imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Mkoa wa Arusha baada ya kuipa kipigo cha mbwa mwizi Laibon ya Longido kwa mabao 9-1 katika mchezo wa mwisho wa hatua ya sita bora ya Ligi ya Mkoa wa Arusha.
Ushindi huo umeifanya AFC kufikisha pointi 11 sawa na Mana FC, lakini ikanufaika na idadi kubwa ya mabao ikiwa nayo 17 ya kufunga na matatu ya kufungwa wakati Mana wana tisa ya kufunga na hawajafungwa hata moja.
Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid Kaluta mjini hapa mwishoni mwa wiki, hadi mapumziko AFC walikuwa wanaongoza kwa mabao 4-0 yaliyofungwa na Erick Daudi, Mgona Kifaru na Jamal aliyefunga mawili.
Kipindi cha pili, AFC walikuja na nguvu zaidi na kujipatia mabao matano zaidi yaliyofungwa na Alidina Hashim kwa penalti, Samson Mwalukwa, Abbas Nkuba na Jamal tena aliyefunga mawili.
Nafasi ya pili imeshikwa na Mana FC ikifuatiwa na Arusha Meat, Flamingo, Suye na timu iliyoshika mkia ni Laibon.
Mgeni rasmi katika mchezo huo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Nyirembe Sabi, ambaye aliwazawadia kombe AFC, ambao sasa watauwakilisha Mkoa katika ligi ya mabingwa wa mikoa.
Aidha, kwa kutwaa ubingwa huo, AFC imezawadiwa sh milioni 50 kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, ambaye aliahidi kutoa kiwango hicho kwa timu yoyote itakayotwaa ubingwa wa mkoa, huku wadau wa michezo wa Arusha wakiahidi kuiunga mkono ili irejee Ligi Kuu.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa