MAMLAKA
ya Mapato Tanzania (TRA), inatarajia kuongeza kiwango cha
wafanyabiashara wakubwa kutoka 23,000 wa sasa hadi kufikia 200,000, ili
kupandisha kiwango cha mapato cha sasa. Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki
na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu Wa TRA, Richard Kayombo wakati
akizungumza na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari Jijini Arusha.
Alikuwa akielezea umuhimu wa matumizi ya mashine kielektroniki (EFDs) za TRA kwa wafanyabiashara.
Alisema
kuna umuhimu wa kuongeza idadi ya wafanyabiashara hao hadi kufikia
kiwango hicho, ili kuongeza mapato ya taifa zaidi ya sasa.
"Hii
mashine inasaidia kujenga nchi kwa kulipa kodi na inaondoa usumbufu wa
makadirio ya mauzo yao, kwani hii inakadiria moja kwa moja, lakini pia
kila anayenunua baada ya mauzo yake ataona faida zake," alisema Kayombo.
Alisema
kwa sasa ugomvi walionao mkubwa ni makadirio ya gharama halisi,
wanazotakiwa kutoa wafanyabiashara kwa TRA na wengi hudai wanabambikiwa
gharma kubwa, tofauti na mauzo halisi.
"Sasa
tukaona bora tulete kifaa hiki ambacho hakina kuchakachua kwa njia
yoyote ile, inasema kweli unachouza ndicho kinachotolewa, ila hapa
muhimu kila mtu anaponunua bidhaa yoyote mdai risiti, sababu huko
tuendako utatozwa faini ya shilingi milioni moja kama hujadai
risiti,"alisema.
Kayombo
alisema pia ili kuleta uhamasishaji wa utoaji risiti na wanunuzi kudai
risiti, muda si mrefu wanatarajia kuleta shindano litakaloshindaniwa kwa
tiketi za zawadi nono.
"Tunataka
kufanya hivi ili kuhamasisha watu kudai risiti na mfanyabiashara kutoa
risiti ili mwisho wa siku wote tupate faida,"alisema.
Alisisitiza
kuwa sio busara kuacha kudai risiti, kwa sababu unapoiacha unamnufaisha
mfanyabiashara husika na wewe mnunuzi unakosa haki yako kimsingi, kwani
bidhaa unayonunua tayari imekatwa kodi.
Chanzo;Habari Leo
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment