Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe.
Mradi huo umegharimu Sh. milioni 930 ili kuhudumia wakazi wapatao 40,000 wa mji wa Karatu na vitongoji vyake.
Akitembelea mradi huo jana, Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, alisema: “Nimefurahi kuona wakazi wa Karatu sasa wameanza kupata maji safi na salama ya kunywa na kwa matumizi mengine ya nyumbani baada ya kukamilika kwa mradi huo uliotekelezwa kwa pamoja kati ya Auwsa na Wizara ya Maji.”
Maghembe pia aliwapongeza wakazi wa Karatu, viongozi wa serikali za mitaa, wahandisi wa Auwsa, Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Karatu kwa kazi kubwa waliyoifanya bila kuchoka katika kuhakikisha mradi huo unakamilika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Auwsa, Mhandisi Ruth Koya, alisema mradi huo umekamilika kwa asilimia 60 na kwa miezi michache mradi huo unatarajiwa kutoa huduma kwa asilimia 81 ya wakazi wa Karatu.
Akirejea agizo la Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alilotaka mradi huo kupanuka na kuwahudumia wakazi wa vijiji viwili zaidi vya jirani, Mhandisi Ruth, alisema, vijiji hivyo vitaingizwa katika awamu ya pili ya mradi huo na hadi wakati huo utaweza kutoa huduma kwa asilimia 90.
Alisema kabla ya mradi huo, asilimia 18 tu ya wakazi wa Karatu ndio walikuwa wakipata huduma ya maji ya bomba lakini kwa sasa huduma hiyo imeweza kufikia asilimia 60.
Chini ya mradi huo, visima viwili virefu vimechimbwa na kuwekewa mashine kubwa za kupampu maji pamoja na vioski ambavyo wananchi wanavitumia kuchotea maji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Karatu, Moses Mabula, alisema katika awamu hii ya kwanza mradi huo umeruka vijiji viwili vya Gyekrum Lambo na Gongali ambavyo vitafikiwa katika awamu ya pili ambayo itaanza mara tu baada ya kukamilika kwa awamu hii ya kwanza.
Mapema Waziri Maghembe aliutaka uongozi wa wilaya na mamlaka zake kuanzisha Bodi ya Maji itakayowahusisha wakazi wa hapo ambayo itawajibika kwa mradi huo kama sheria ya maji inavyotaka.
Alisema bodi hiyo pamoja na mambo mengine ndiyo itakayohusika na masuala ya kupanga bei ya maji.
Aliahidi kutumia mradi huo wa Karatu akisema kuwa ni mfano wa kuigwa ambapo umewahusisha kikamilifu wakazi wake.
Alisema atatumia mfano wa Karatu kutekeleza miradi ya maji katika miji mingine ya Ngudu mkoani Mwanza, Buselesele wilayani Chato na Uramba mkoani Tabora.
SOURCE:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment