KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) inakusudia
kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria baadhi ya watendaji katika
Halmashauri ya Wilaya ya Longido mkoani Arusha kutokana na
kinachoelezwa kushindwa kutekeleza maagizo ya kamati hiyo.
Akitoa maagizo ya kamati wakati wa hitimisho la ziara ya siku mbili
wilayani humo, Kaimu Mwenyekiti wa LAAC, Suleiman Zedi, alisema kamati
hiyo haikuridhishwa na utekelezaji wa baadhi ya miradi pamoja na
utendaji kazi wa baadhi ya watumishi katika halmashauri hiyo.
Zedi aliwataja watendaji wanaopaswa kufikishwa mbele ya vyombo vya
sheria kuwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Charles Chalya,
Ofisa Mipango Miji, Joan Fuya na Mhandisi wa Maji, Edwin Rwezaura
ambao wanadaiwa kuwa watovu wa nidhamu kwa kamati na walipakodi.
Alisema watendaji hao wameidanganya kamati katika taarifa ya mradi wa
maji ya kusukuma wa Kisima cha Tembo katka Kijiji cha Longidoya kuwa
wananchi wanapata maji, suala ambalo si la kweli na kwamba baada ya
ukaguzi kamati iligundua kuwa hakuna maji yanayotoka katika mradi huo.
“Mkurugenzi na watu wako tutawafikisha mbele ya vyombo vya sheria
siku ya majumuisho ya ziara yetu katika Mkoa wa Arusha yatakayofanyika
Februari 6 kutokana na kuonyesha utovu wa nidhamu kwa kamati hii,”
alisema Zedi.
Awali akisoma taarifa ya mradi mbele ya kamati hiyo, Mhandisi wa Maji
wa Halmashauri, Rwezaura, alisema kiasi kilicholipwa kwa mkandarasi
baada ya kufanya tathmini ya kazi halisi iliyofanyika ni sh milioni 253
huku kiasi kilicholipwa kwa mhandisi mshauri ni sh milioni 38.6.
Alipotakiwa kutoa ufafanuzi endapo kisima hicho kinatoa maji,
mhandisi huyo alisema maji yanatoka suala ambalo lilipingwa na walinzi
wa kisima hicho na mwenyekiti wa halmashauri.
Walipohojiwa walinzi hao walisema hawajawahi kuona maji yakitoka
katika kisima hicho wala wananchi kupata maji walau hata mara moja.
Chanzo;Tanzaia daima
0 comments:
Post a Comment