Mbunge wa Arusha Mjini wa Chadema, Godbless Lema.
Mpango huo ulitangazwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Mbunge wa Arusha Mjini wa Chadema, Godbless Lema.
Lema alisema chama hicho kimeishiwa uvumilivu kutokana na kikundi hicho kuendesha vitendo hivyo tangu kuanza kwa kampeni zake za kumnadi mgombea wao.
Alisema matukio ya kuvamiwa na kupigwa kwa wafuasi wa chama hicho yamezidi kukithiri kutokana na polisi kushindwa kuwachukulia hatua kali dhidi ya kikundi hicho.
Lema alisisitiza kuwa Chadema hakitasubiri kibali cha polisi cha kufanya maandamano, bali kitatoa taarifa ya kuwapo kwake ili kufikisha kilio chao na kuiwezesha dunia kufahamu kuwa Arusha bado si shwari .
''Juzi mfuasi wetu amekatwa panga kichwani na kufyekwa vidole,tumetoa taarifa polisi ,hakuna hatua zozote zilizochukuliwa,tupeleke wapi kilio chetu , tumeona bora tuandae maandamano ya amani kulaani matukio hayo,'' alisisitiza Lema.
Alisema wao kama wafuasi na wanachama wa Chadema wapo tayari kukamatwa kwa kuandamana kupinga unyanyasaji unaofanywa dhidi yao.
Kwa mujibu wa Lema, hadi sasa zaidi ya wafuasi 50 wa Chadema wamejeruhiwa vibaya na magari matano kuharibiwa kwa kuvunjwa vioo. Hadi juzi matukio saba yametokea tangu kampeni hizo ambazo zilianza Januari 15, mwaka huu na hakuna mtu aliyekamatwa kwa kuhusishwa nazo.
Alimtuhumu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha , Liberatus Sabas kuwa ameonyesha chuki za dhati dhidi yake na Chadema kwa sababu amekuwa hapokei simu yake anapompigia kumtaarifu matukio ya uhalifu yanayoendelea katika kampeni hizo.
Kwa upande wa Kamanda Sabas, akizungumza kwa njia ya simu na NIPASHE alikana tuhuma za kumchukia Lema na kwamba ndiye aliyetangaza kutompigia simu hata kama atavamiwa na majambazi.
''Ndugu zangu mimi simchukii mtu yoyoye kwanza huyo kijana (Lema)aliwahi kutangaza kwamba, hatanipigia simu yangu hata kama atavaamiwa na majambazi, sasa hapo nani anamchukia mwenzake, ''alihoji Kamanda Sabas.
Akizungumzia kuhusu vurugu za Sombetini, alisema hajapata taarifa kamili na kusisitiza hakuna aliyejuu ya sheria.
Alisema iwapo kama kuna mtu ameripotiwa kwa kuhusika na uvunjifu wa amani, atakamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment