MIGOGORO ya wafugaji na wakulima katika Tarafa ya Enduimeti, Wilaya
ya Longido, mkoani Arusha imedhibitiwa baada ya Hifadhi ya Taifa ya
Mlima Kilimanjaro (Kinapa), kutoa elimu kwa makundi hayo ikiwamo
hifadhi ya mazingira na kuepuka ufugaji wa kuhamahama.
Pamoja na hilo, lakini pia tatizo la baadhi ya wafugaji kutelekeza
familia zao kwa kigezo cha kutafuta malisho limemalizika baada ya
hifadhi kuanzisha miradi ya kiuchumi kwa lengo la kuwasaidia wafugaji
na wakulima.
Ofisa Uhusiano wa hifadhi hiyo, Theodory Lois, alisema hayo wakati
akikabidhi mradi wa mbuzi wa maziwa kwa wanawake wa kikundi cha Upendo
ambapo pia wamefanikisha maji ya bomba katika Kata ya Kamwanga, ujenzi
wa zahanati ya Kijiji cha Irkaswa kuanzisha vikundi vya uzalishaji mali
na ufugaji wa kisasa.
“Ile tabia ya kuwapo kwa migogoro ya wafugaji na wakulima sasa
itakuwa imekwisha maana hii miradi itawawezesha kukaa eneo moja,
kitendo cha kuhamahama kilikuwa kikiwagombanisha na wakulima, tunzeni
hii miradi lakini pia otesheni miti ya kutosha,” alisema.
Alisema Kinapa imefanikiwa kudhibiti uharibifu mkubwa wa mazingira
katika hifadhi hiyo baada ya wafugaji katika Tarafa ya Enduimeti
kusitisha ufugaji wa kuhamahama na kujikita katika fursa za ujasirimali
na ufugaji wa kisasa.
Diwani wa Enduimeti, Neema Lee, alipongeza wafugaji kwa kukubali
kusitisha utaratibu wa kutafuta malisho kwa kuhamahama kutaibadili
jamii hiyo kuwa ya kisasa zaidi.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment