Serikali imesema itaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) hususan za kuhamasisha wananchi
kujiunga na mfuko huo pamoja na Mfuko wa Afya wa Jamii (CHF) ili
wanufaike na huduma za matibabu.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Maendeleo
ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk Pindi Chana wakati alipotembelea banda la
NHIF katika Maadhimisho ya Miaka 50 ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii
Tengeru ambayo yamekwenda sambamba na Mkutano Mkuu wa Maofisa Maendeleo
ya Jamii nchini.
Katika maadhimisho hayo, NHIF inatoa huduma za
upimaji wa afya bure, kutoa elimu ya namna ya kujikinga na maradhi
yasiyoambukiza pamoja na elimu inayolenga faida za kuwa katika utaratibu
wa kupata matibabu kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Mfuko wa
Afya ya Jamii na Tiba kwa Kadi.
Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Hamis
Mdee, alitumia mwanya huo kuwaomba Maofisa Maendeleo ya Jamii
kuhamasisha wananchi kujiunga na mifuko hiyo kwa kuwa ndio njia pekee ya
kumkomboa mwananchi na kumfanya awe na uhakika wa kupata matibabu
wakati wowote.
“Mtaji wa mwananchi yoyote ni afya yake mwenyewe,
huwezi ukafanya shughuli zozote za kimaendeleo bila kuwa na afya njema,
gharama za matibabu kwa sasa ni kubwa hivyo njia ya uhakika na rahisi ni
kujiunga na mifuko hii na kwa upande wetu kama NHIF tunaendelea na
uboreshaji wa huduma zetu ili kuondokana na changamoto chache zilizopo,”
alisema Mdee.
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Maofisa
Maendeleo waliofika katika banda la NHIF, waliupongeza mfuko kwa kuweka
huduma hiyo ambayo imewasaidia kujua afya zao, pia kupata majibu ya
maswali waliyokuwa nayo kuhusiana na huduma zinazotolewa na NHIF.
Akizungumza bandani hapo Elias Lotaa alisema ni
wakati sasa kwa NHIF kuhakikisha inakwenda zaidi katika maeneo ya
vijijini kuhamasisha wananchi kujiunga na Mifuko hii kwa kuwa inayo
manufaa makubwa.
“Mimi ni shuhuda mzuri wa huduma nilizopata kutoka
NHIF, gharama nilizolipiwa kwa ajili ya matibabu ya mke wangu ni kubwa
ambayo kwa hali ya kawaida ingeniwia ngumu sana hivyo nawahamasisha sana
wananchi kujiunga na Mfuko huu lakini na nyie NHIF ongezeni bidii ya
kufikia makundi mengi wakiwemo wakulima na wafugaji,” alisema.
Akizungumzia mkakati wa elimu kwa umma, Kaimu
Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti, Christopher Mapunda alisema kuwa NHIF
inaendelea na mikakati mbalimbali ya elimu ikiwemo ya Elimu ya kata kwa
kata ambayo inawafikia wananchi wengi zaidi.
Alisema kuwa suala la utoaji wa elimu kwa NHIF ni
endelevu hivyo akawaomba wananchi kutumia fursa zilizopo kujiunga na
huduma za Mifuko hii. “Kwa sasa tumesogeza sana huduma kwa wananchi kwa
kufungua ofisi katika mikoa 25 hivyo tunaamini changamoto nyingi za
wanachama wetu zinatatuliwa kwa uharaka,” alisema Mapunda.
Chanzo ;Mwananchi
Chanzo ;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment