BARAZA
la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Arusha jana lilikuja juu na
kutaka kauli kutolewa juu ya ni hatua gani zichukuliwe kuhusu walimu
wakuu wa shule za msingi na sekondari wanaowachangisha wazazi fedha
kabla ya mtoto kuanza darasa la kwanza na wanaojiunga kidato cha kwanza.
Diwani
wa TLP, Michael Kivuyo ndiye aliyeanzisha mjadala huo kwa kutoa hoja
binafsi iliyoungwa mkono na karibu madiwani wote na kusema kuwa watoto
wanarudishwa shule iwapo hawatakuwa wametoa kiasi cha fedha
kinachopangwa na Mwalimu Mkuu.
Kivuyo
alisema mbali ya hilo hata mtoto aliyefanikiwa kufaulu na kuingia
Kidato cha Kwanza naye ana michango yake na iwapo michango hiyo
haitatolewa na wazazi, watoto hawaruhusiwi kuanza shule ya msingi na
kidato cha kwanza.
Alisema
na kuwaeleza Madiwani kuwa; “watoto wanarudishwa shule na walimu wakuu
kwa kushindwa kulipa michango hiyo ambayo sijui fedha zake zinafanya
nini na zinaingia katika fungu lipi kwani Serikali ilishapiga marufuku
suala la michango holela isiyokuwa ya kisheria.”
Diwani
huyo alisema kuwa Baraza la Madiwani limekuwa likiagiza kila mara
katika vikao vyake juu ya walimu wakuu kuacha mara moja kuchangisha
wazazi michango hiyo lakini walimu hao wakuu wamekuwa wajeuri na wakaidi
kwa kushindwa kutekeleza amri na maagizo ya Baraza tangu mwaka juzi na
aliliomba Baraza kutoa kauli juu ya hilo ili iwe mwisho kwa walimu
kuchangisha.
‘’Walimu
wakuu wamekuwa miungu mtu kwani wanachangisha fedha bila ya utaratibu
na wanawarudisha watoto majumbani ambao wanashindwa kutoa michango hiyo
hivyo naomba Baraza kutoa kauli juu ya walimu wakuu,’’ alisema.
Naye
Diwani wa Sekei kupitia Chadema, Crispin Tarimo yeye alioneshwa
kusikitishwa na hali hiyo na kusema kuwa wananchi wameshoshwa na
michango hiyo isiyokuwa na utaratibu na kuwataka madiwani kuiunga hoja
hiyo na kutolea maamuzi mazito juu ya walimu wakuu wenye tabia ya
kukaidi amri ya Baraza na Serikali Kuu.
Tarimo
aliendelea kusema Serikali Kuu iliagiza kuwa hakuna mtoto
atakayerudishwa shule kwa kukosa michango na Baraza la Jiji la Arusha
katika vikao vyake liliagiza hivyo hivyo lakini agizo hilo limeshindwa
kutekelezwa na walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari za Jiji la
Arusha.
Diwani
wa Lemara CCM, Karimu Mushi alizungumza kwa masikitiko makubwa na
kusema kuwa wazazi na wananchi wanabebeshwa mzigo mkubwa ambao hauko
kisheria hivyo aliomba Baraza kuangalia hilo kwa faida ya baadaye.
Diwani
wa Terrat CCM , Julius ole Sekayani yeye aliwaunga mkono madiwani wote
walitoa hoja na kuchangia na kumtaka Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha,
Gaudence Lyimo na Baraza kuthubutu kuchukua hatua juu ya ukaidi wa
walimu wakuu hao.
Akizungumzia
kauli za madiwani hao, Meya Lyimo alimtaka Mwenyekiti wa Kamati ya
Elimu, Afya na Uchumi kuchukua hoja hizo na kuzifanyia kazi na kutoa
taarifa katika kikao kijacho cha Baraza uamuzi ambao baadhi ya madiwani
walionekana kuupinga. Meya Lyimo alisema; “
Hata
mimi suala hili la walimu wakuu kukaidi linanisikitisha na hapa nataka
kujiridhisha zaidi, naomba niipe kazi kamati hiyo ifanye kazi na kutoa
mapendekezo katika kikao kijacho.”
Chanzo;Habari Leo
0 comments:
Post a Comment