Arusha
Home » » Lema, Nassari kuzindua kampeni Sombetini

Lema, Nassari kuzindua kampeni Sombetini

Godbless Lema na Joshua NassariWABUNGE wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Arusha, Godbless Lema na Joshua Nassari, wanatarajia kuzindua kampeni za udiwani Kata ya Sombetini, kesho.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, mgombea wa kata hiyo, Ally Bananga, alisema kutokana na ratiba ya kampeni ya vyama vya siasa iliyotolewa na ofisi ndogo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), uzinduzi huo utafanyika katika viwanja vya Mbauda Mnadani.
Bananga alisema maandalizi ya uzinduzi huo yanaendelea vizuri ili kuhakikisha mkutano huo unafanikiwa na kuvunja rekodi ya mikutano yote iliyowahi kufanyika ya chaguzi ndogo za udiwani kwa vyama vyote.
“Makamanda wote wa mkoa, wilaya na kata wanaendelea na maandalizi ya uzinduzi na mikutano mingine ili tuweze kuichukua Kata ya Sombetini Februari 9 mwaka huu… tuna imani mkutano huo utakuwa mkubwa kuliko yote ambayo ilishawahi kufanyika,” alisema.
Hata hivyo, wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa wanasema uchaguzi huo unatarajiwa kuwa na mnyukano mkali kati ya mgombea wa CHADEMA, Bananga na David Leskar wa CCM, mtoto wa aliyekuwa mwenyekiti wa zamani wa kata hiyo kutokana na historia ya vyama hivyo jijini humo.
NEC ilitangaza kufanyika uchaguzi katika kata 27 nchini ambazo zipo wazi kutokana na madiwani wake kufariki dunia na wengine kupoteza sifa.
Katika hatua nyingine, Bananga alisema hadi sasa Jeshi la Polisi mkoani humo bado halijawaita kuwahoji wala kuwakamata waliohusika na uvamizi wa msafara wake Januari 15, mwaka huu wakati akirejesha fomu za kuwania nafasi hiyo.
Bananga alisema kundi la vijana wanaowasadiki kuwa ni wafuasi wa CCM, walivamia gari aina ya Toyota Hillux mali ya katibu mwenezi wa chama chao wilaya, Emanuel Kombe, na kuwapiga waliokuwamo na kuvunja vioo.
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa