MGOGORO
wa uongozi mkoani Arusha umefikia hatua mbaya ambapo sasa ni wazi
Mkurugenzi wa Jiji, Sipora Liana, hawezi kuiva chungu kimoja na Mkuu wa
Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Meya na Baraza la Madiwani. Mkuu wa Mkoa, Magesa
Mulongo amegonga mwamba baada ya Liana kupuuza agizo lake alilotaka
litekelezwe ndani ya siku sita.
Mulongo
mwishoni mwa Desemba, alimtaka Liana aombe radhi kwake, kwa Mkuu wa
Wilaya ya Arusha, John Mongela na Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha,
Gaudence Lyimo kwa madai ya kuwadharau, lakini hadi jana hajafanya
hivyo.
Mulongo
alisema katika kikao hicho cha kutathimini miradi inayotekelezwa chini
ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, kuwa Liana asipoomba radhi atakuwa
tayari kumpisha mkoa.
Wakati
Mulongo akisubiri kauli ya Liana kuomba radhi, jana Mkurugenzi huyo
alionesha nguvu, alipoamuru wakuu wa idara na watendaji wa Halmashauri,
wasuse kikao cha Baraza la Madiwani.
Kususa
Kabla ya kuamuru watendaji kususa Baraza, Liana akiwa katika kikao
hicho, Diwani Cyprian Tarimo aliomba kikao kibadilike kuwa Kamati ili
kujadili tuhuma zinazomkabili Mkurugenzi huyo kutoka kwa madiwani.
Naibu
Meya wa Halmashauri ya Jiji, Prosper Msofe, alitoa fursa kwa madiwani
kupiga kura ya kukubali au kukataa hoja hiyo, ndipo madiwani wakaafiki
Mkurugenzi ajadiliwe.
Baada ya maafikiano hayo, Liana alisimama na kuamuru wakuu wa idara na watendaji wote wa Halmashauri watoke nje ya kikao hicho.
Akizungumzia
hali hiyo, Msofe alisema walibadilisha Baraza kuwa Kamati kwa kufuata
kanuni ya 13(a) na kanuni ya 2 ambazo zinaruhusu kama madiwani wana
jambo la kulishughulikia wafanye hivyo.
“Sisi
tumefuata kanuni na sheria, lakini hatukufanikiwa kuendelea na kamati
kwa sababu Katibu kisheria ni Mkurugenzi ambaye amezira kwa sababu zake,
ila tulichofanya tumeandika malalamiko yetu na kupeleka kwa Mkuu wa
Mkoa,” alisema Msofe.
Alisema
wakiwa katika Kamati hiyo, walituma wenyeviti wa kamati mbili ya
Mipango Miji na Uchumi, Elimu na Afya wakamwite Mkurugenzi aje
kusikiliza kero za madiwani, akatoa jibu kwa maandishi kuwa hawawezi
kumjadili na kimsingi kikao hicho ni batili.
“Sasa
kama sisi tumejibiwa hivyo, basi tumeandika malalamiko yetu na
yatakwenda kwa Mkuu wa Mkoa kama sheria inavyosema,” alisema Msofe.
Meya
Meya Lyimo, alisema Baraza lilipoanza alikuwa akiaga mwili wa kijana
aliyefariki dunia Mererani ambaye ni jirani yake na alimruhusu Naibu
Meya kuendelea na kikao. Alisema alipomaliza kuaga, alikwenda kwenye
Baraza hilo na kukuta limebadilika kuwa kamati.
“Sasa
kama kimsingi Mkurugenzi alitakiwa kujibu hoja za madiwani na yeye
akakimbia, basi sisi tumeorodhesha kero zetu na tutapeleka kwa Mkuu wa
Mkoa ambaye ana mamlaka ya kuitisha kikao cha dharura cha Baraza na hapo
mtasikia yote,” alisema Lyimo.
Aliongeza kuswa Mkuu wa Mkoa yupo kwa niaba ya Rais na hivyo wanatarajia yote yafanyike, ili watendaji wote wawekane sawa.
“Mnajua
hapa hatuwezi kufanya kitu chochote na hatuwezi kuitisha tena kikao
chochote bila Mkuu wa Mkoa kufanya hivyo, kwa sababu hapa viongozi tuna
tofauti za kiutendaji na ni tatizo,” alisema Lyimo.
Kuhusu
kutoelewana kwake na Mkurugenzi wa Jiji, Lyimo alisema hana ugomvi ila
ana tofauti za kiutendaji na wangependa wawekwe sawa ili wafanye kazi.
Diwani wa Sokoni One, Michael Kivuyo, alisema Mkurugenzi amedharau
madiwani kiasi cha kuwaandikia barua kuwa hawawezi kumjadili, wakati
uwezo wa kumjadili wanao, ila uamuzi utatolewa na mamlaka zingine.
“Sisi tuna uwezo wa kumjadili na leo tumejadili kero zake kwetu ila kuna mamlaka za kutoa uamuzi,” alisema Kivuyo.
Waandishi
walipojaribu kwenda kwenye ofisi za Mkurugenzi kusikiliza upande wake,
hakutaka kuonana nao na badala yake alituma mjumbe aliyedai kuwa
hahitaji kuzungumza na yeyote na hana cha kusema.
Chanzo;Habari Leo

0 comments:
Post a Comment