Home » » Wafanyabiashara wapigwa stop kupanga bidhaa nje ya maduka yao‏

Wafanyabiashara wapigwa stop kupanga bidhaa nje ya maduka yao‏

Na Mwandishi wetu-Arusha yetu Blog
Mkuu wa mkoa wa Arusha Magesa Stanslaus Mulongo ametoa siku saba kwa wamiliki wa maduka jijini hapa kuacha mara moja tabia ya kupanga bidhaa zao nje ya maduka yao.

Aliyasema hayo wakati akizungumza na viongozi wa Serikali za mitaa pamoja na wakuu wa idara mbalimbali wa jiji la Arusha.

Mulongo alisema kuwa tabia ya baadhi ya wafanyabiashara kupanga bidhaa nje ya maduka ni kinyume na sheria na hali hiyo inapelekea kuonekana kama hakuna mipango madhubuti ya kufanya biashara zao na kuonekana kama jiji ni chafu.

Aidha amewataka wakuu wa idara kusimamia sheria zilizopo kwa kuhakikisha hakuna pia mfanyabiashara yeyote anapanga bidhaa nje na sio kwa maduka tu bali pia kwa wafanyabiashara ndogondogo wa soko la kilombero na soko kuu jijini hapa.

“wakuu wa idara naomba msiangalie kula  tu lakini pia msimamie sheria zilizopo kwa kushirikiana na viongozi wa serikali za mitaa watendaji wote,wenyeviti wa vijiji na vitongoji sheria ndio ifanye kazi msiendekeze kula yenu tu”alisema Mulongo

Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa oparesheni hiyo itakuwa ni ya kudumu kwa kuwa hali hiyo ya kufanya biashara pembezoni mwa barabara mbali na kufanya jiji kutokuwa na mpangilio na kuonekana chafu lakini pia  ni hatari pindi gari linapokosea njia.

Amesema kuwa ili kuepuka usumbufu ni vyema wafanyabiashara wa maduka wakaweka vibao pembezoni mwa maduka yao kwa ajili ya kutangaza bidhaa zilizopo huku wale wa masoko ya kilombero na soko kuu kutumia soko la ndani ili kupunguza usumbufu utakaojitokeza kwa wafanyabiashara wa ndani kutoka nje kwa madai wateja wanaishia nje.

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa