Home » » RC aamuru wajenzi kukamatwa kwa tuhuma za kuhujumu mil. 213/-

RC aamuru wajenzi kukamatwa kwa tuhuma za kuhujumu mil. 213/-

Mkuu wa Mkoa Arusha,Magesa Mulongo
 
Mkuu wa Mkoa Arusha, Magesa Mulongo, ameamuru kukamatwa kwa wafanyakazi watatu wa kampuni ya ujenzi ya Winning  Sprit, kwa tuhuma za  kuhujumu  Sh. milioni 213 za mradi wa maji vijiji vya Patanumbe na Kikuletwa vya halmashauri ya Meru, wilayani Arumeru.
Wafanyakazi hao ni John Petro, Maximilium Markely na Mathias Bombo, huku mhandisi mshauri wa kampuni ya Howard Hamphreys (T) Ltd, Zena Kiwanga na mwenzake Kaimu mhandisi wa maji, Maningo Mohamedy, wakiamuriwa kwenda polisi kutoa maelezo jinsi kampuni hiyo ilivyohujumu mradi huo.

Watuhumiwa hao walikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi wilayani Arumeru, Athumani Nyange, wakati alipokuwa kwenye ziara ya siku moja ya ukaguzi wa miradi ya  Matokeo Makubwa sasa (Big Result Now) inayofanyika katika halmashauri ya Meru.

Akizungumza mara baada ya kuamuru kukamatwa kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo, Mulongo alisema miradi hiyo ilipaswa kukabidhiwa Desemba 27, mwaka huu, baada ya kuingia mkataba wa miezi sita tangu Juni, lakini hadi sasa kazi iliyofanyika ni asilimia 20, huku wakijizolea milioni 213 na jumla ya mradi wote una thamani ya Sh. bilioni  1.2.

“Huu ni wizi mkubwa ubabaishaji umewajaa na Kiswahili kingi, siwezi kufanya kazi na makandarasi wababaishaji katika mkoa wangu, askari kamata hawa peleka polisi maana wamehujumu mradi wa wananchi na kula fedha za wahisani za serikali,” alisema Mulongo.

Aidha, alisema kuwa kazi walizotakiwa kufanya kijiji cha Patanumbe ni kutoa maji safi na salama kwa kujenga pampu ya kusukuma maji na kituo cha kuhifadhi pampu hiyo, uwekaji wa umeme wa kusaidia kuendesha pampu, utandazaji bomba kubwa la kusambaza maji la kilomita 19.88, ujenzi wa vilula 22  (vituo vya kuchotea maji), ujenzi wa tanki la juu ya jukwaa la mita sita na ujenzi wa matanki ya uvunaji maji ya mvua yenye ujazo wa lita 5,000,  3,000 na 2,000.

Huku kijiji cha Kikuletwa kilitakiwa kujengwa kituo cha kuhifadhia pampu ya kusukuma maji, uwekaji umeme wa Tanesco, utandazaji bomba kuu la kusambazia maji kijijini leye urefu wa kilomita 9.38, wa vilula 20 (vituo vya kuchotea maji), wa tanki la juu la mita sita lenye ujazo wa 135, tanki la uvunaji maji ya mvua lenye uwezo wa lita kati ya 5,000 na 2,000.

Awali  Mbunge wa Jimbo  la Arumeru Mashariki, Joshua Nasari, akiambatana na mkuu wa mkoa, alimwomba  kuchukua hatua kali dhidi ya kampuni hiyo kwa kuchelewesha kumaliza kazi.

Nassari alisema wananchi wa eneo hilo wanahitaji maji safi na salama  kwa haraka, hivyo kuchelewesha mradi ni sawa na mauaji.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Makiba, Mwanahidi Kimu alimwomba Mulongo kushinikiza ili mradi umalizike kwa wakati, kwani matumaini ya mradi kuisha Desemba hayapo, kutokana na Mhandisi kufanya kazi kwa kusua sua na kusukumwa.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa