MAONESHO ya madini ya vito na bidhaa za usonara yaliyofanyika jijini Arusha hivi karibuni na kuwashirikisha wafanyabiashara wakubwa duniani yameingiza dola milioni 4.397 za Marekani (sh bilioni 6.9) kama mauzo ya madini hayo.
Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini, Benjamini Mchwampaka,
alibainisha hayo mjini hapa jana na kusema pia serikali ilifanikiwa
kupata sh milioni 227.4 kama malipo ya mrahaba, pamoja na kuingiza
nchini na kutoa madini hayo imefanikiwa kupata zaidi ya dola 200 za
Marekani.
Maonesho ya mwaka jana yaliingiza dola milioni 3.8 ambayo ni sawa na sh bilioni 6.
“Maonesho hayo yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani wafanyabishara wa
Kitanzania wameweza kupata fursa ya kukutana na wafanyabiashara
wakubwa wa madini duniani,” alisema Mchwampaka.
Alisema wafanyabishara wa madini kutoka Tanzania na Afrika kwa jumla
walikuwa 180, wakiwakilisha makampuni 54 toka nchi 10 ambazo ni
Tanzania, Kenya, DRC, Madagasca, Msumbiji, Zambia, Afrika Kusini,
Nigeria na Uganda.
Kutoka nchi za Ulaya na Asia, walikuwepo wanunuzi 160 kutoka nchi 24
duniani ambazo ni Marekani, Italia, Ufaransa, Ujerumani Australia,
Ugiriki, China, Thailand na Austria.
Hata hivyo Kamishna Mchwampaka alisema maonesho ya tatu yatafanyika
jijini Arusha, kati ya Novemba 18 hadi 20 mwakani. Maonesho hayo
yanaandaliwa na serikali kwa kushirikiana na Chama cha Wauza Madini
Tanzania (Tamida).
0 comments:
Post a Comment