Monduli:Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema waliofurahi na kuhuzunika naye pia watashinda pamoja naye.
Bila kufafanua kauli yake jana, Lowassa aliwaambia
wakazi wa Monduli mkoani Arusha kuwa: “Kumbukeni kaulimbiu yangu wakati
wa Uchaguzi Mkuu uliopita, tulifurahi pamoja, tulihuzunika pamoja na
tutashinda pamoja”.
Mbunge huyo wa Monduli alikuwa akizungumza kwenye
mkutano wa hadhara mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa wodi
mbili za ghorofa za wazazi katika Hospitali ya Wilaya ya Monduli.
Katika hotuba yake fupi, pia alitamba kwamba
atayashinda majaribu. Hata hivyo, hakufafanua majaribu hayo... “Kuna
vita kubwa, lakini ambacho naweza kusema ni kuwa nayaweza yote kwa yeye
anitiaye nguvu.”
Kuhusu afya yake ambayo mara kadhaa imeelezwa kuwa
siyo imara, kiongozi huyo alisema kwa sasa ni nzuri na imeimarika
kupita kipindi kingine chochote.
Lowassa alisema kuanza ujenzi wa majengo hayo
ambayo ni utekelezaji wa ahadi zake, ni moja ya ushindi na kuwataka
wakazi wa Monduli, kumshukuru Mungu kwa yanayotokea.
Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Arusha, Onesmo
Nangole aliwataka wakazi wa Monduli, kumshukuru Mungu kwa kuwa na mbunge
Lowassa ambaye anapendwa nchi nzima.
“Monduli Mungu awape nini, Lowassa anaitwa kila
mahala kusaidia kutokana na moyo wake wa huruma na hapa ametekeleza
ilani yote ya uchaguzi,” alisema.
Kauli ya Lowassa imekuja siku chache tangu
mtangulizi wake katika nafasi ya Waziri Mkuu, Frederick Sumaye
alipomtuhumu hadharani kwamba amekuwa akimhujumu na kumwekea vikwazo vya
kisiasa kwa kutumia mbinu chafu. Miongoni mwa mambo yaliyoonekana
kumkera Sumaye ni habari iliyoandikwa na gazeti hili Septemba 16, mwaka
huu inayohusu mradi wa maji Ziwa Victoria, ambayo Lowassa alinukuliwa
akisema kuwa wakati akiwa Waziri wa Maji, aliungwa mkono na mawaziri
watatu tu alipopendekeza mradi huo wa maji.
Sumaye alisema: “Najua mhusika ametumia sana mradi
huu kisiasa na sisi wengine tumenyamaza japo ukweli tunaujua.
Amenilazimisha niseme ukweli kuhusu mradi huu kwa sababu mimi nilikuwa
Waziri Mkuu na mradi umetekelezwa chini ya uangalizi wangu,” alisema na
kuongeza:
“Kama waziri anaweza kubuni na kutekeleza mradi
mkubwa hivyo peke yake, sasa akiwa Waziri Mkuu si maji yangefika Dodoma?
Mbona hata bado kuna sehemu za Kanda ya Ziwa bado kuna shida ya maji?”
Tangu Sumaye atoe tuhuma hizo ambazo zinahusishwa
na vita ya kuwania urais wa 2015, Lowassa hakuwahi kujibu chochote wala
kusikika akizungumza hadharani, hadi jana.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment