Home » » Lema atakiwa achome moto picha chafu

Lema atakiwa achome moto picha chafu

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema)
 
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), amesema amezigawa picha za kutengeneza zinazomdhalilisha kwa wachungaji 50 na kwamba anatarajia kufanya hivyo kwa masheikh ili wasaidie kukemea siasa chafu ambazo zimeanza kwa kupitia mitandao ya kijamii.
Hata hivyo, mamia ya wanachama walikataa kugawiwa picha hizo juzi jioni katika mkutano wa hadhara badala yake walikubaliana zichomwe moto.

Lema hata hivyo, alisema picha hizo haziwezi kumrudisha nyuma yeye pamoja na chama chake katika harakati za kuchukua dola mwaka 2015.

Alikuwa akizungumza katika mkutano alioufanya juzi jioni, pamoja na mambo mengine, Lema alizungumzia kuhusu uchungu alioupata wa kudhalilishwa kwenye mitandao ya kijamii kwa kutumia picha iliyotengenezwa ikimuonyesha akifanya matendo ambayo yanakiuka maadili ya jamii.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na mkewe, Neema, awali alipanga mkewe awagawie wanachama picha hizo, lakini kabla ya kufanya hivyo, alitaka kupata ridhaa yao kwanza.

“Kabla ya kuwagawia hizi picha naomba niwaulize, nizigaweee,” nao wakamjibu kwa sauti, “achaaa’. Baadaye Lema aliuliza tena na kupewa jibu hilo hilo, na kisha akasema, “Nimeelewa hisia zenu na ninaziheshimu.”

Hata hivyo, Lema aliwaambia wapigakura wake kuwa amepeleka picha hizo kama ushahidi kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda na Naibu Spika, Job Ndugai, kama vielelezo vya kudhalilishwa na watu hao.

PROF. TIBAIJUKA NAYE ALALAMIKA
Mbali na Lema, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, naye amelalamika katika kikao cha Baraza la Madiwani cha Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera, kwamba amekuwa akichafuliwa na mahasimu wake kisiasa kupitia mitandao ya jamii.

Akizungumza katika kikao hicho, alisema: “Wapo baadhi yetu kwa kushirikiana na vijana wetu tunatumia vibaya mitandao ya kijamii kuchafuana, kila nikifanya jambo hata likiwa ni la kiujamaa, kifamilia lakini linatafsiriwa visivyo, lakini tutambue kwa kuendeleza hayo si kuijenga halmashauri yetu, wana Muleba inatubidi kushikamana, nimekuwa nikiwasiliana nanyi madiwani, lakini mtambue mimi nawapenda japo baadhi yenu hamnipendi … itakula kwenu.”

Ingawa hakuwataja waliotumia vibaya mitandao ya jamii dhidi yake, lakini Julai mwaka huu baadhi ya mitandao iliwekwa habari kuhusiana na waziri huyo.

TCRA YAJIWEKA PEMBENI
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejiweka pembeni kwa kusema kuwa haihusiki katika kudhibiti vitendo vya watu kuwadhalilisha wengine kwa kutumia mitandao ya kijamii.

Mamlaka hiyo ilitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa kufuatia tukio la Lema kudhalilishwa na watu wasiojulikana kwa kutumia mitandao ya jamii.

Akizungumza na gazeti hili jana ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Meneja wa Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungy, alisema mamlaka hiyo haishughulikii masuala kama hayo isipokuwa wenye mamlaka ni Jeshi la Polisi.

Kwa mujibu wa Mungy, TCRA inashughulikia masuala nyeti yakiwamo ya usalama wa nchi na kudhibiti kampuni za mawasiliano ya simu kwa upande mwingine.

Aliongeza kuwa, vitendo hivyo vya uhalifu vimekithiri kwa wingi kwenye mitandao ndani na nje ya nchi na kwamba mbali na tukio la Lema, wapo viongozi wengi nchini ambao nao pia wamechafuliwa vivyo hivyo.

Mungy aliongeza kuwa hata kwa ngazi ya kimataifa hakuna sheria rasmi inayoelekeza kuwadhibiti watu wanaohusika na vitendo hivyo.

KAULI YA POLISI
Naye Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso, alipotakiwa na NIPASHE kuzungumzia suala hilo, alimtaka mwandishi aende ofisini kwake leo ili ampe maelezo zaidi kwa ajili ya kuujulisha umma juu ya udhibiti wa vitendo hivyo vya uhalifu wa kwenye mitandao.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa