Arusha.Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) mkoani Arusha, kimewafungulia mashtaka mengine ya madai
madiwani wake watano waliofukuzwa uanachama mwaka juzi na kuwataka
walipe Sh35 milioni ikiwa ni gharama za usumbufu.
Kesi hiyo ilifunguliwa katika Mahakama Kuu Kanda
ya Arusha kwa Msajili wa Mahakama hiyo. Kwa mara ya kwanza kesi hiyo
ilitajwa mwishoni mwa wiki iliyopita.
Hii ni kesi ya pili kufunguliwa na Chadema dhidi ya madiwani hao.
Novemba mwaka jana, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha
mbele ya Hakimu Charles Magesa ilitoa hukumu ya kuwataka walipe Sh15
milioni ikiwa ni gharama za usumbufu wa kuondoa shauri lao mahakamani
kupinga kufukuzwa katika chama hicho.
Katika kesi iliyofunguliwa hivi karibuni kwenye
mahakama hiyo, iligawanywa mara mbili; Dai la kwanza ni Sh20 milioni na
dai la pili ni Sh15 milioni.
Chama hicho katika kesi hiyo nambari 34 na 35 ya
mwaka 2013, pia imefungua madai dhidi ya madiwani hao na kuwataka
wakilipe kwa madai kuondoa shauri walilofungua dhidi ya chama hicho
mahakamani hapo kwa kupinga kufukuzwa sanjari na kuomba kupunguziwa
kiwango cha fedha walichopaswa kulipa mahakamani hapo.
Madiwani waliofukuzwa ni Estomih Mallah, Rehema Mohammed, John Bayo na Ruben Ngowi wanaowakilishwa na Wakili Gwakisa Sambo.
Wadaiwa hao walihudhuria kusikilizwa shauri hilo,
lakini Charles Mpanda hakuonekana mahakamani hapo na kesi hiyo itatajwa
tena Desemba 4 mwaka huu.
Chadema kiliwafukuza madiwani hao kikiwatuhumu
kukisaliti baada ya kuingia makubaliano ya kugawana madaraka na CCM,
kuongoza Manispaa ya Arusha.
Uongozi wa chama hicho ulipinga mchakato wa
kumpata Meya wa Jiji la Arusha, Gaudence Lyimo kikidai haukuwa halali na
haki. Madiwani hao bila ridhaa ya chama chao walikubaliana na CCM
kugawana madaraka, lengo likiwa ni kuondoa mgogoro uliosababisha na
matokeo hayo.
Hata hivyo, walikwenda mahakamani kupinga kufukuzwa uanachama, lakini walishindwa na uchaguzi uliporudiwa Chadema ilishinda.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment