Moshi.
Suala la mgawanyiko wa madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi,
limechukua sura mpya baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji,
Genesis Kiwelu kufungua taarifa Polisi akidai kutishiwa kuuawa.
Mgawanyiko huo unatokana na madiwani walio wengi
kuwashtukia wenzao wawili kwamba wanacheza mchezo mchafu wa kutaka kumpa
mwekezaji mmoja eneo la katikati ya mji bila masilahi ya Halmashauri
kuwekwa wazi.
Kiwelu ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ng’ambo
(Chadema), alipokea vitisho hivyo kupitia ujumbe mfupi wa maandishi
(SMS) uliotumwa kwenye simu yake ya mkononi na watu wasiojulikana wiki
iliyopita.
Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi,
wamegawanyika katika makundi mawili huku wengi zaidi wakipinga utaratibu
wa chini kwa chini wa kutaka kumpa mwekezaji eneo lililopo katikati ya
mji wa Moshi.
Moja ya SMS hiyo inasomeka; ”Mheshimiwa Kiwelu
hatukuamini kuwa wewe ni mtu mbaya na ovyo namna hiyo na sasa
tutakuonyesha na utatujua sisi ni akina nani…Unajitia hutaki rushwa huku
unanuka shida”.
SMS nyingine inasomeka”Ukisikia watu wanachomewa
nyumba ama kumwagiwa tindikali ni mambo ya kipuuzi namna hii,
nakuhakikishia tutakufanyizia”, SMS zinazodaiwa kutumwa na kundi
linalomuunga mwekezaji. Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Robert Boaz
hakupatikana jana kuelezea sakata hilo, lakini Kiwelu mwenyewe
alipotafutwa alilithibitishia gazeti hili na kwamba alifungua jalada la
uchunguzi Kituo cha Polisi Majengo.
“Ni kweli nimetumiwa hizo meseji na namba
nisiyoijua na ukiipiga haipatikani… Polisi waliniambia jalada
litahamishiwa ofisi ya RCO (mkuu wa upelelezi) lakini nahisi kiini ni
hilo suala la uwekezaji”alisema Kiwelu.
CHANZO;MWANANCHI.
0 comments:
Post a Comment