MKURUGENZI wa Kampuni ya Afrika Amini Alama iliyopo katika
Hifadhi ya Momela jijini Arusha, Dk. Christine Wallner, amesema kuwa
wana mpango wa kuanzisha kituo cha tiba ya asili, ikiwa ni mbinu mpya
za matibabu ya asili kutoka nchini Austria, ambayo itawasaidia
wagonjwa wengi wakiwamo wa ukimwi.
Kituo hicho maalumu kwa tiba ya asili kinatarajiwa kuwasaidia wana
jamii ya Wamasai na Wameru wanaoishi katika vijiji vya Ngabobo na
Ngarenanyuki, Mkoa wa Arusha na mikoa mingine na hata nchi jirani.
Tayari taratibu za kuanzisha kituo hicho zimeshaanza, ikiwamo
kupeleka maombi katika Wizara ya Afya na kupata eneo ambalo litatumika
kujenga kituo hicho pamoja na wataalamu waliobobea katika fani hiyo.
Dk. Christina akizungumza na waandishi wa habari, alisema kuwa kituo
hicho kitasaidia wagonjwa wa mifupa, uti wa mgongo na kuwasaidia
wagonjwa wa ukimwi kuimarika kiafya.
“Tunahitaji kufanya kazi pamoja na serikali kwani imekuwa ikiridhia
jitihada tunazozifanya hata tulipoanza na ujenzi wa zahanati ya
kijiji ambayo ina chumba kidogo cha upasuaji, wodi na leba, ambapo
tayari imeanza kutumika,” alisema Dk. Christine.
Mbali na hayo, mkurugenzi huyo ameweza kujenga Shule ya Masai Vision
Primary School, Afrika Amini Sports Academy, kituo cha afya, Afrika
Amini Training Center na kuanzisha kikundi cha Umoja wa Kina Mama
Wazalishaji (Women Group).
Kwa upande wake, Dk. Christine alisema kuwa miradi ya maendeleo ya
jamii iliyoanzishwa imewasaidia watoto 550 kusoma bure na kupata
udhamini wa mahitaji yao muhimu kama chakula, malazi na vifaa vya shule
na bado wanaendelea kuangalia namna ya kuisaidia jamii inayowazunguka
na vijiji vya jirani.
chanzo;tanzania daima
|
0 comments:
Post a Comment