Arusha
Home » » `Tunachunguza tukio la kupigwa risasi mwanamke aliyeitishia polisi bastola`

`Tunachunguza tukio la kupigwa risasi mwanamke aliyeitishia polisi bastola`

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas
Utata umeendelea kugubika tukio la kupigwa risasi na kujeruhiwa Violeth Mathias Lyapa, anayedaiwa kutishia polisi kwa bastola baada ya kuegesha gari lake kwenye lango la kuingilia benki ya CRDB tawi la Mapato eneo ambalo haliruhusiwi kufanya hivyo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema jana kuwa jeshi lake linafanya uchunguzi wa tukio zima ili kujua hatua gani za kisheria zinaweza kuchukuliwa.

Kwa sasa Violeth amelazwa Hospitali ya Rufaa ya Selian ambako amewekewa ulinzi unaowazuia watu wengine isipokuwa ndugu wa karibu kwenda kumuona wakati polisi aliyempiga anaendelea na kazi.

Kamanda Sabas alidai kuwa hakuna polisi waliowekwa hospitalini hapo kumlinda, lakini alisisitiza kwamba upelelezi wa tukio hilo unaendelea.

Tukio la kujeruhiwa kwa Violeth lilitokea Jumatano iliyopita na tangu wakati huo habari zake zimekuwa ngumu kutolewa na wahusika hadi jana Kamanda Sabas, alipolazimika kufanya hivyo baada ya waandishi wa habari kumsubiri ofisini kwake kwa zaidi ya saa moja.

Hata hivyo, Kamanda Sabas alipotakiwa kueleza iwapo Violeth anamiliki bastola hiyo kihalali, alidai kuwa anamiliki kihalali tangu Januari 28, mwaka huu.

Huku akikataa kutaja namba ya bastola, Kamanda Sabas aliishia tu kusema imetengenezwa Czechoslovakia, (kwa sasa nchi hiyo imesambaratika).
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa