WASHITAKIWA watano akiwamo askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU)
jana wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani hapa
wakikabiliwa na kesi ya wizi wa sh milioni 228, mali ya Kampuni ya
ujenzi ya Dott Service Ltd.
Tukio hilo lililotokea Oktoba 29, mwaka huu, majira ya saa 4 asubuhi
katika maungio ya barabara za Arusha na Old Boma Manispaa ya Moshi,
wakati Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Shuresh Bab (45) yeye na wafanyakazi
wengine wakipeleka fedha hizo katika Benki ya NMB, Tawi la Mandela baada ya kuzitoa Benki ya Standard Charted.
Wakili wa Serikali, Oscar Ngole, alimweleza Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
Mahakama hiyo, Simon Kobelo, kwamba watuhumiwa wanaokabiliwa na kesi
hiyo ni Francis Mushi (27) maarufu kama Master ambaye ni mtunza stoo
wa Kampuni ya ujenzi ya Dott Service na mkazi wa Kibosho-Longuo A.
Aliwataja wengine kuwa ni Wenceslaus Mambo (36) ambaye ni dereva wa
Kampuni ya ujenzi ya Dott na mkazi wa Kariwa chini pamoja na askari
polisi mwenye namba Ex. G. 1674 PC Jackson Nzengule (28) maarufu kama
King, mkazi wa Mabogini.
Wengine ni Philbert Lyimo (33) maarufu kama Kadogoo, dereva wa
bodaboda na mkazi wa Longuo ‘A’ katika Manispaa ya Moshi na Jackson
Brayson, maarufu kama Rema, mfanyabiashara wa njia panda, Wilaya ya
Moshi.
Wakili Ngole, akiwasomea mashitaka yao watuhumiwa hao, alisema kwenye
kosa la kwanza, siku na tarehe isiyojulikana nchini Tanzania,
watuhumiwa hao walikula njama ya kutenda kosa kinyume na kifungu cha
384 cha kanuni ya adhabu, sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka
2002.
Ngole aliieleza mahakama kuwa kosa la pili ni la wizi wa kutumia
silaha, kinyume cha kifungu cha 287A cha kanuni ya adhabu ya mwaka 2002
ambayo imefanyiwa marekebisho katika sheria namba nne (4) ya mwaka
2004 ambapo washitakiwa walitumia silaha aina ya bastola kuwatishia
maofisa wa Kampuni ya ujenzi ya Dott ili kufanikisha wizi huo. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 22, mwaka huu.
Chanzo;Tanzania Daima
|
0 comments:
Post a Comment