SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (TANAPA) limeamua
kubadili mfumo wake wa utendaji kazi kutoka wa kiraia na kuwa wa kijeshi kwa
watumishi wote ili kuongeza umakini katika kukabiliana na ujangili.
Tayari bodi ya mamlaka hiyo, imeishapitisha uamuzi
huo na kuuwasilisha serikalini ili kupata ridhaa. Sasa watumishi wote
watalazimika kupata mafunzo rasmi ya kijeshi ili kuendelea kuwepo kazini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, meneja
mahusiano wa Tanapa, Pascal Shelutete alisema uamuzi huo umetokana na
changamoto kubwa iliyopo sasa ya ujangili katika hifadhi za taifa.
Alisema katika jitihada za kukabiliana na ujangili
ndani ya hifadhi za taifa, kwa kipindi cha miezi miwili ya Aprili na Juni,
askari wa Tanapa waliweza kukamata silaha za moto 85 toka kwa majangili na 795
za kienyeji.
Alitaja aina ya silaha zilizokamatwa kuwa ni
civilian rifle saba, magobore 60, automatic rifle tano na short-gun 13. Pia
waliweza kutegua nyaya za kutegea wanyama 25,422.
Shelutete alisema licha ya kubadili mfumo wa
watumishi, hata mfumo wa ajira sasa wameubadili. Wameanza kuajiri askari kutoka
Jehi la Kujenga Taifa (JKT) na Chuo cha Wanyamopori cha Pasiansi, Mwanza.
Alisema kuwa wanaofaulu katika usaili wanakwenda
katika mafunzo maalumu ya kisasa kukabiliana na ujangili.
Kwa mujibu wa Shelutete, kwa kuanzia tayari kuna
askari 100 waliofuzu usaili wa awali, na wanapelekwa katika mafunzo maalumu ya
mbinu za medani yatakayofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Katavi na
watakaofuzu, wataajiriwa rasmi na shirika hilo.
Aliongeza kuwa wapo baadhi ya watumishi wa Tanapa
wanashirikiana na majangili, na kwamba uchunguzi umeanza kwa wale wote
waliotajwa, na ikithibitika hatua ya kwanza itakuwa ni kufukuzwa kazi na
baadaye kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Alisema hali ya kudhibiti ujangili inakuwa ngumu
kutokana na soko kubwa la vipusa lililoko katika nchi za China, Thailand na
Malaysia. Kwamba wafanyabiashara wakubwa hutoa ufadhili maalumu kufanikisha
ujangili ndani ya hifadhi.
Shelutete aliongeza kuwa wameanzisha kikosi maalumu
kilichopata mafunzo ya kisasa ya mbinu za medani chenye askari 40 kwa ajili ya
kukabiliana na matukio ya uhalifu.
Alisema tayari kikosi hicho kimeanza kutoa
mafanikio. Kwa miezi sita toka kimeanza kazi, hakuna tukio lililotokea katika
hifadhi ya Ruaha ambako kimeanzia.
Katika hifadhi za Tarangire na Ziwa Manyara,
alisema kwa miezi sita sasa hakujaripotiwa taarifa za kuuawa kwa tembo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment