SHIRIKA la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO)
limeitaka Kampuni ya kuchakata umeme ya Symbion Power (T) Ltd kuhakikisha
inarekebisha mitambo yao iliyopo Njiro jijini hapa ili kudhibiti sauti na moshi
unaodaiwa kuwa na kemikali.
Tayari wakazi wa eneo hilo wamelalamikia mitambo hiyo
wakidai kuwa inahatarishia afya zao, na hofu ya kupata ugonjwa wa saratani
kutokana na moshi mkubwa mweusi unaotanda angani sanjari na sauti na mitetemeko
inayosababisha nyufa kwenye nyumba zao.
Kaimu Mkurugenzi wa TANESCO, Felchesmi Mramba
aliyasema hayo alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari mara baada ya
kufunguliwa kwa mkutano wa muungano wa wasambazaji na wazalishaji wa vifaa vya
umeme wa nchi za kusini mwa Afrika (PIESA).
Alisema kuwa mkataba wa Symbion na TANESCO wa
kuzalisha umeme wa dharura ambao alidai kuwa gharama yake ni kubwa, unatazamiwa
kumalizika mwezi Oktoba mwakani, hivyo akawaomba wananchi hao kuwa wavumilivu
kwa kipindi hicho.
Mramba alisema kuwa baada ya kipindi hicho mitambo
hiyo itaondolewa kwenye eneo hilo huku akisisitiza kuwa tayari alishaongea na
uongozi wa kampuni hiyo ili kuhakikisha wanairekebisha ili kuwapunguzia kero
wananchi.
Awali wananchi hao kutoka vitalu B, C, na D
walishapeleka malalamiko yao kwenye taasisi mbalimbali ikiwemo Baraza la Taifa
la Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), wakilalamikia athari za kimazingira
zinazosababishwa na mitambo hiyo inayozalisha megawati 66 iliyowekwa kwenye
kitalu C bila wao kushirikishwa.
Wanadai kuwa eneo hilo lililokuwa likitumiwa na
TANESCO kusambaza umeme lilibadilishwa matumizi na kuanza kuzalisha umeme bila
kuwashirikisha wala kufanyiwa tathmini ya mazingira kama sheria inavyotaka.
Malalamiko ya wananchi hao yanaungwa mkono na
majibu ya NEMC ambao pamoja na mambo mengine waliwaeleza wananchi hao kuwa
tathmini ya kimazingira ilikuwa haijafanywa kwenye eneo hilo kama sheria
inavyoagiza.
Akizungumzia mkutano huo, Mramba ambaye ndiye
mwenyekiti wa PIESA, alisema kuwa ni muhimu kwani utawawezesha washiriki
kubadilishana uzoefu wa kitaalamu kupitia tafiti zilizofanywa ili kurahisisha
zoezi la uzalishaji, usambazaji na ugavi wa umeme.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Steven Masele
alisema kuwa wamejipanga kuongeza mtandao wa umeme hapa nchini kutoka asilimia
21 za sasa hadi asilimia 30 ifikapo 2015.
“Asilimia saba kati ya 21 ya mtandao wa umeme hapa
nchini uko vijijini, tumeamua kuweka nguvu kubwa ya kusambaza umeme vijijini
kupitia wakala wa usambazaji umeme vijijini (REA). Hadi kufikia mwakani
tutakuwa tumevifikia vijiji 1,600 na vile vile vilivyoko mjini vitaunganishwa
na TANESCO,” alisisitiza Masele.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment