Mkuu wa Kitengo cha
Polisi Jamii Mkoa wa Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Mary Lugola
akihutubia wananchi wakati wa siku ya maadhimisho ya Mtoto wa Mtaani
iliyofanyika tarehe 12/04/2013 katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliopo mjini
Arusha. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Baadhi ya wanafunzi wa
shule ya Msingi mojawapo iliyopo Mkoani Arusha wakiwa wanashiriki mashindano ya
kukimbia kwa kutumia magunia yaliyofanyika mapema katika siku ya kuadhimisha
Mtoto wa Mtaani iliyofanyika tarehe 12/04/2013 kwenye uwanja wa Sheikh Amri
Abeid mjini Arusha. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Na Rashid
Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi la Polisi Mkoani hapa limesema
litaendelea kushirikiana na mashirika mbalimbali katika kulinda na kutetea haki
za watoto. Hayo yalisemwa na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Mary Lugola ambaye
pia ni Mkuu wa Kitengo cha Polisi Jamii Mkoa wa Arusha mwishoni mwa wiki
iliyopita wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa mtaani duniani.
Katika maadhimisho hayo ambayo
yalifanyika tarehe 12 mwezi huu katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini hapa,
Mrakibu huyo Mwandamizi wa Polisi alisema kwamba jeshi la polisi kupitia dawati
la jinsia na watoto mkoani hapa limekuwa karibu sana kiutendaji na mashirika
mbalimbali yasiyokuwa ya serikali kama vile Mkombozi, CCR, Action For Children
n.k katika kutetea na kulinda haki za watoto wa mitaani.
Mrakibu huyo Mwandamizi wa Polisi
ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Polisi Jamii Mkoa wa Arusha alisema mbali na
jeshi hilo kujihusisha katika kutetea na kulinda haki za watoto wa jamii hiyo,
pia linasaidia kuinua na kuibua vipaji vya watoto hao kupitia programu ya
MWONGORIKA ya Polisi jamii ambayo inajihusisha na michezo kwa vijana.
Alisema kupitia Dawati hilo, jeshi
la polisi limeweza kuwahudumia watoto wa mitaani kwa kushirikiana na mashirika
hayo ili kuwawezesha waishi katika mazingira salama na kupata mahitaji muhimu.
“Kwa mfano tumeshawahi
kuwaunganisha na wazazi wao pamoja na kuwasafirisha kwenda makwao watoto
waliokuwa tayari kurudi ”. Alisema Bi. Lugola.
Alimalizia kwa kusema kwamba Dawati
la Jinsia na watoto huwa linahakikisha linapata taarifa za watoto walioathirika
na pia wale wote wanaowanyanyasa watoto hao wanachukuliwa hatua za kisheria
ikiwemo kufikishwa mahakamani.
Nalo shirika la Mkombozi kupitia
risala yao iliyosomwa na Afisa Ustawi wa Jamii wa Shirika hilo Bi. Doris
Cornell alisema kwamba ujumbe wa mwaka huu katika kuadhimisha siku hiyo ni
“Nyumbani Mtaani Nyumbani” ikiwa na maana ya kwamba, mtoto atatoka nyumbani
kwenda mtaani na kisha atarudi nyumbani.
Alisema lengo la siku hiyo ni kuwapa
jukwaa watoto waishio na kufanya kazi mtaani wakiungana na wengine duniani kote
kupaza sauti ili haki zao zisiipuzwe.
Bi. Doris alisema watoto waishio
mitaani na kulala mitaani wanazofursa na haki sawa na watoto wengine duniani na
kwamba wana haki ya kuishi, kulindwa, kuendelea na kushiriki katika mambo
yanayogusa maisha yao kama ilivyoainishwa katika mkataba wa Kimataifa wa haki
za watoto kifungu cha 4.
Risala hiyo ilieleza sababu za
kuwepo kwa watoto hao mitaani ni pamoja na kukosa haki za msingi (chakula,
malazi, mavazi, ulinzi, elimu, upendo, matibabu n.k) kutoka katika familia zao,
kufiwa na mzazi mmoja au wote wawili,
Sababu nyingine ni vitendo vya
unyanyasaji na ukatili waliofanyiwa katika jamii au familia, kipato duni katika
familia/wazazi/walezi, utumikishwaji wa watoto (ajira za watoto), kubaguliwa na
kunyang’anywa mali za wazazi wao.
Siku hiyo ambayo huwa inaadhimishwa
katika nchi 130 duniani, Tanzania na Uingereza ikiwa ni miongoni mwa nchi hizo,
ilihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa ngazi ya wilaya pamoja na Mkuu wa
Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Arusha Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Maria
Maswa.
0 comments:
Post a Comment