Mkurugenzi wa Kampuni ya Emags Video Entertainments Bw.
Elias Magesa akiongea na waandishi wa habari (Hawapo pichani) huku pembeni yake
ni Kaimu Kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP)
Ibrahim Kilongo akimsikiliza wakati kampuni hiyo ikikabidhi radio 16 za
mkononi kwa Jeshi la polisi Mkoani Arusha ( Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la
Polisi Arusha)
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la
Polisi Arusha
Jeshi la Polisi mkoani hapa jana
limepokea radio za mkononi 16 ambazo zilitolewa na Kampuni ya Emags Video
Entertainments iliyopo jijini hapa. Akitoa radio hizo, Mkurugenzi wa Kampuni
hiyo Elias Magesa alisema kwamba, wameamua kutoa radio hizo ili ziweze
kurahisisha mawasiliano ndani ya jeshi hilo.
Bwana Magesa alisema radio hizo
zenye thamani ya Tsh 2.6 Mil. zitaweza kulisaidia jeshi hilo kuimarisha ulinzi
katika shughuli zake za kila siku. Alisema kupitia mawasiliano kutawezesha
askari kuwasiliana na hatimaye kufanikisha kuimarisha ulinzi katika maeneo
mbalimbali ya mkoa huu.
“Suala la Ulinzi si la jeshi la
Polisi pekee bali ni la watu wote ndio maana kwa kutambua hilo Kampuni yetu ya
EMAGS Video Entertainments imeaua kutoa radio hizo kwa jeshi hilo kwani kwa
kufanya hivyo naona tutakuwa tumeshiriki kwa namna moja au nyingine katika
dhana ya ulinzi shirikishi”. Alifafanua Bw. Magesa.
Kwa upande wake Kaimu Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Ibrahimu Kilongo
akipokea radio hizo kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini alitoa shukrani
zake kwa kampuni hiyo na kuongeza kwamba, amefarijika sana na moyo ulioonyeshwa
na Bw. Elias Magesa pamoja na kampuni yake kwani si wote wanaoweza kufanya
hivyo.
“Kutoa ni moyo si lazima uwe na
kitu kikubwa sana ndipo utoe unaweza kuwa na chochote na ukatoa kama kampuni
hii ilivyofanya. “ Alisema Kaimu Kamanda huyo.
Alisema radio hizo zimepatikana
muda muafaka kwani bado kuna changamoto ya upungufu wa vitendea kazi na
kuongeza kwamba zitasaidia sana katika kuimarisha hali ya usalama kwani
zitakuwa zinatumika na askari wa jeshi hilo katika doria na maeneo mbalimbali
hali ambayo itasaidia kuimarisha mawasiliano.
Kaimu Kamanda Kilongo alitoa
wito kwa wadau wengine wa mkoa huu kuiga mfano wa Kampuni hiyo kwa kujitokeza
kuchangia vitendea kazi vitakavyosaidia kurahisisha utendaji ndani ya jeshi
hilo.
Naye Afisa Uhusiano wa Kampuni
hiyo Bw. Severinus Mwijage alisema pamoja na
kujishughulisha na utengenezaji wa filamu lakini pia wameona wawe karibu na
Jamii ambao ni wadau wao wakubwa kwa kutoa radio hizo ambazo zitasaidia
mawasiliano ya ndani ya jeshi la polisi na hatimaye kuimarisha ulinzi katika
maeneo ya wananchi hao.
0 comments:
Post a Comment