Home » » DK. ASHA MIGIRO KUWASILI ARUSHA

DK. ASHA MIGIRO KUWASILI ARUSHA

Na Mwandishi Wetu, Arusha

ALIYEKUWA Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Dk. Asha Rose Migiro, anatarajiwa kutua jijini Arusha kuzindua Baraza la Viongozi Wakuu wa Serikali za Mitaa la Afrika Mashariki.

Dk. Migiro pia atafungua mkutano wa Mawaziri wa Serikali za Mitaa na Viongozi wa juu wa Serikali za Mitaa kutoka Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, wanaokutana mjini Arusha kwa mara ya kwanza.

Taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) iliyosambazwa jana, ilidai lengo la kuzinduliwa baraza hilo ni kufanya kazi kwa pamoja katika kuimarisha utendaji wa Serikali za Mitaa.

“Uzinduzi wa mkutano huo utafanyika Septemba 24, mwaka 2012 na kufungwa Septemba 25, mwaka huu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo iliendelea kubainisha kuwa, kupitia mkutano huo, viongozi wa Serikali za Mitaa watapata nafasi ya kubadilishana uzoefu kuhusu namna ya uwakilishi wa wananchi unavyofanyika.

Ilizitija nchi zitakazoshiriki katika mkutano huo kuwa ni nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambazo ni Burundi, Kenya, Rwanda, Tanzania na Uganda.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa nchi za Visiwa vya Comoro na Sudan ya Kusini nazo zimealikwa kushiriki. Washiriki wengine wa mkutano huo ni wadau wa maendeleo ambao ni Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Mkutano huu umefadhiliwa na Serikali ya Tanzania, nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Jumuiya ya Madola sehemu ya Serikali za Mitaa na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa