Na Nicodemus Ikonko,
Hirondelle
Mwendesha mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa ya
Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) ameiomba mahakama hiyo iwatie hatiani kwa
tuhuma nyingine walizoachiwa huru wafungwa wawili, akiwemo Waziri wa zamani wa
Vijana wa Rwanda, Callixte Nzabonimana na afisa wa zamani wa jeshi la nchi
hiyo, Ildephonse Nizeyimana.
Katika taarifa fupi ya rufaa dhidi kesi ya Nzabonimana, mwendesha
mashitaka anaiomba Mahakama ya Rufaa kuachana na uamuzi uliotolewa na mahakama
ya awali kuhusu matukio ya uhalifu yaliyofanywa Aprili 15 na 17, 1994 katika
wilaya za Nyabikenke na Rutobwe katika mkoa wa Gitarama, katikati ya Rwanda.
Mei 31, 2012, mahakama ya awali ilimtia hatiani Nzabonimana kwa mauaji
ya kimbari,kula njama za kufanya mauaji hayo,uchochezi na kuteketeza kizazi
katika matukio mengine na kumhukumu kifungo cha maisha jela, lakini aliachiwa
huru kwa uhalifu uliofanyika katika maeneo hayo mawili yanayotajwa na mwendesha
mashitaka.
Kwa mujibu wa mwendesha mashitaka katika rufaa yake ya Septemba 12,
2012, anadai kwamba majaji wa mahakama ya awali wamekosea kisheria kwa kumwona
Nzabonimana kuwa alichochea tu mauaji yaliyofanyika katika ofisi za wilaya ya
Nyabikenke Aprili 15, 1994, badala ya kumtia hatiani kwa kushiriki au kuamuru
kufanyika kwa mauaji hayo.
Mwendesha mashitaka anadai kwamba majaji wangemtia hatiani Nzabonimana
pia kwa kosa la kusaidia na kuunga mkono mauaji dhidi ya Watutsi katika wilaya
ya Rutobwe Aprili 17, 1994, kwa kusababisha kuachiwa huru watuhumiwa wa mauaji
waliotiwa kizuizini na maafisa wa serikali za mitaa kutokana na vitendo vyao.
Lakini majaji walimwachia huru kwa kosa hilo kwa maelezo ya kukosa ushahidi wa
kutosha.
Kwa upande wa Kapteni Nizeyimana, mwendesha mashitaka anataka atiwe
hatiani pia kutokana na nafasi yake kama kiongozi wa askari waliodaiwa kutenda
uhalifu kwenye Chuo Kikuu cha Butare na Hospitali ya Butare, Kusini mwa Rwanda.
Juni 19, 2012, majaji wa mahakama ya awali walimtia hatiani Nizeyimana
kwa mauaji ya kimbari,uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita katika
maeneo mbalimbali kwenye mkoa huo wa Butare na kuhukumiwa kifungo cha maisha
jela.
NI/FK
© Hirondelle News Agency
© Hirondelle News Agency
0 comments:
Post a Comment