Home » » AGRA YATETEA WAKULIMA WADOGO AFRIKA

AGRA YATETEA WAKULIMA WADOGO AFRIKA

Na Eliya Mbonea, Arusha



JUKWAA la Mapinduzi ya Kijani Afrika (AGRA) limesema endapo wakulima wadogo wa Afrika wakipatiwa zana za kilimo, uwezekano wa kukua na kuongeza kipato chao ni mkubwa.

Hayo yalibainika mjini hapa jana, wakati wa mkutano wa waandishi wa habari na Rais wa AGRA, Jane Karuku, juu ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa jukwaa hilo.

“Wakulima wadogo wadogo ni kitovu kwa yale yote tuyafanyayo na mtazamo wetu ni wazi na kuthibitika,” alisema Jane.

Alibainisha kuwa jukwaa hilo litaendelea kujadili na kutafuta njia bora za kuboresha kilimo barani Afrika na kuwawezesha wakulima wadogo kwa kushirikiana na vyama vya ushirika na wadau wengine.

Alisema kupitia mkutano huo wanatarajia mijadala tofauti itatoa njia bora za matumizi ya rasilimali na kukubaliana na changamoto zinazowakabili mamilioni ya wakulima Afrika.

“Mkutano unaoanza Septemba 26 hadi 28 mwaka huu, utalenga kupata ufumbuzi katika masuala ya usalama wa chakula,” alisema Jane na kuongeza:

“Mkutano wa hivi karibuni wa G 8 na viongozi wa kimataifa wa nchi 21 za Afrika na Kampuni 27 za sekta binafsi ziliahidi Dola za Marekani Bilioni 3 kwa ajili ya mpango mpya wa usalama wa chakula na lishe ili kuondoa watu milioni 50 katika umasikini kwa miaka 10 ijayo,” alisema.

Jane alibainisha kwamba Tanzania ikiwa mwenyeji wa mkutano huo katika kukuza sekta ya kilimo na ukuaji wa kilimo, inawakilisha uchunguzi uliofanywa katika wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro juu ya njia bora za kilimo.

Alisema ukuzaji huo umewezesha uzalisha wa mahindi kwa wakulima wadogo wilayani humo kuongezeka kutoka tani 1.5 hadi 4.5 kwa hekta, na mavuno ya mpunga yaliweza kuongezeka kutoka tani 2.5 hadi tani 6.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa