Joseph Lyimo, Karatu
WAKULIMA wa Kijiji cha Rhotia, wilayani Karatu mkoani Arusha wamelalamikia kutolipwa fedha zao za ardhi na Raia wa Uholanzi walizokubaliana kulipwa kwa kuwaachia ardhi yao.
Wanakijiji hao ikiwamo familia ya Pili Basu ambaye ni mjane walimtaja raia wanayemdai kuwa ni Malise Koch Hekstra anayemiliki kambi ya kulaza wageni ya Rhotia Valley Children Home &Tented Lodge LTD.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa niaba ya wenzake Basu alisema kuwa tangu mwaka 2006 uongozi wa kambi hiyo uliomba ardhi kutoka kwa wanakijiji hao kwa lengo la kupanua eneo lake na kukubaliana kwa mdomo kwa ahadi ya kulipwa fedha na kuwatafutia wananchi hao eneo jingine.
Basu alisema kuwa tangu Juni mwaka 2006 familia hiyo imekosa eneo la kilimo hivyo kukosa chakula changamoto inayosababisha watoto wa familia hiyo kushindwa kulipiwa karo baada ya mwekezaji huyo kukataa kuwalipa eneo hata fedha.
“Hivi sasa siwezi kulima katika shamba langu, familia yangu inateseka yeye amejenga kambi na shamba tulilobadilishana naye sina uwezo wa kulirejesha..ninahisi uchungu familia yangu haina chakula na watoto wangu sina uwezo wa kuwalipia karo..badhi ya viongozi wa serikali ya kijiji wamekuwa wakimtetea,” alisema.
Basu alisema kutwaliwa kwa ardhi yake yenye ukubwa wa ekari sita kimetokana na Rais wa Asasi ya Rhotia Valley Tented Lodge& children’s Home kumwomba eneo hilo kwa ahadi ya kuinufaisha familia yake huku pia wakitumia lugha ya kiingereza katika mazungumzo ambayo hawakuielewa.
“Walikuwa wakizungumza kwa lugha ya Kiingereza ambayo hatukuwa tukielewa mambo mengi na sisi tulikuwa tukikubali baada ya kutafsiriwa, kumbe nia yao ilikuwa ni kutupora ardhi yetu. Tunapomuuliza rais wa asasi hiyo naye anadai amefukuzwa na raia huyo na hatakiwi kufika,” alisema.
Rais wa asasi hiyo Mosses Makalla alikiri kuomba ardhi na kuchonga barabara kupita kwenye eneo hilo chini ya asasi ya Rhotia valley children’s Home and Lodge iliyolenga kuwahudumia watoto yatima,lakini baada ya kukamilika raia huyo walitofautiana na kubadili jina la asasi hiyo kuwa Rhotia Valley Tented Lodge & Children’s Home Limited.
“ Tulipotofautiana alilazimisha kuchukua uongozi kwa nguvu na mimi niliondoka kwenda nje ya nchi. Nimerudi na nimesikia mama huyo anasumbua pale na kutofautiana na wanakijiji, nilitegemea Idara ya Uhamiaji ingejaribu kufuatilia, kujua uhalali wake, lakini imesuasua mpaka leo licha ya kufuatilia hadi makao makuu,” alisema.
Hata hivyo baadhi ya viongozi wa Serikali ya kijiji hicho walikubali kuitambua asasi hiyo kupitia muhtasari wa vikao vya mikutano mikuu, lakini wanashangazwa raia huyo kubadili jina la asasi hiyo, kutofutiana na wanakijiji huku akiwa anafanya biashara ya kuuza mikate.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Rhotia Jackson Sulle alisema licha ya kuwepo kwa raia huyo, lakini hatoi ushirikiano wala hatambui kuwepo kwa Serikali ya Kijiji, halmashauri wilaya, wala idara za Serikali hivyo kufanya mambo yake anavyotaka akituhumiwa pia kuingia darasani na kumpiga mwalimu.
Mmoja wa maofisa wa Idara ya Uhamiaji, Elias Shesheda alikiri kumtambua raia huyo kama mwekezaji halali kulingana na vielelezo vilivyopo ambapo amepewa daraja A linalomruhusu pia kufanya biashara zake.
Hata hivyo alisema kuwa yeye si msemaji wa idara hiyo na kutaka asubiriwe ofisa mkuu wa uhamiaji eneo hilo aliyekuwa safarini Moshi kuzungumzia suala hilo.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment