Home » » Chuo chakumbwa na kashfa ya ubaguzi

Chuo chakumbwa na kashfa ya ubaguzi


Na Grace Macha, Arusha


CHUO Kikuu cha Arusha, (UOA) kinachomilikiwa na Kanisa la Sabato nchini (SDA) kimeingia kwenye kashfa kikidaiwa kumbagua mfanyakazi wake, Angelus Ngatunga, baada ya kubaini si Msabato, hivyo kumwandikia barua ya kusitisha ajira yake ifikapo Oktoba 30, mwaka huu.
Ngatunga ambaye ni Mhadhiri Msaidizi aliieleza Tanzania Daima Jumatano kuwa alipewa barua ya ajira ya kudumu Mei 11, mwaka jana lakini alishangazwa na hatua ya uongozi wa chuo hicho kumpa barua nyingine Mei 14, mwaka huu ikimweleza kuwa ameongezewa mkataba wa mwaka mmoja utakaomalizikia Oktoba 30 mwaka huu na hawako tayari kuendelea naye baada ya hapo.
Alisema alipopatiwa barua hiyo alifuatilia kwa Mkuu wa Kitengo cha Rasilimali watu na utawala chuoni hapo, David Wanani ambaye baada ya kumbana kwa maswali alimweleza kuwa uongozi wa chuo ulifikia uamuzi huo baada ya kubaini ni Mkatoliki aliyesoma seminari.
Alisema kuwa Mei 28, mwaka huu aliamua kuijibu barua hiyo na nakala kuipeleka ngazi mbalimbali za uongozi wa chuo hicho ikiwamo Mwenyekiti wa Muungano wa Makanisa ya Sabato nchini (Adventist Church) na Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU).
Kwenye barua hiyo ambayo Tanzania Daima Jumatano inayo nakala yake, Ngatunga alisema aliacha kazi yake ya awali ya uhadhiri msaidizi, Mratibu wa Tafiti na mshauri wa huduma kwenye Chuo Kikuu cha Mtakatifu John cha mjini Dodoma baada ya kuhakikishiwa ajira na uongozi wa UOA.
Makamu Mkuu wa chuo hicho, Emanuel Matiko, alikiri Ngatunga kupatiwa barua ya kuonyesha mkataba wake ukiisha hautahaulishwa huku akidai yeye ni mgeni, kwani ameanza kazi chuoni hapo Februari mwaka huu, hivyo hajui kama mhadhiri msaidizi huyo alikuwa na ajira kamili.
Hata hivyo, alikanusha taarifa za Ngatunga kubaguliwa kwa kuwa si Msababto kwa madai kuwa chuo hicho kina wafanyakazi zaidi ya 30 ambao si Wasabato na wana ajira za kudumu.

Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa