Na Idd Uwesu Arusha yetu
Jumuiya ya Afrika Mashariki imeandaa Semina maalumu kuhusu usimamizi wa rasilimali zinazopatikana ndani ya mipaka ya nchi tofauti kama vile ziwa Victoria na namna ya kutunza mfumo ikolojia wa rasilimali hizo katika nchi za Afrika Mashariki ikiwa na lengo la kujadili namna bora ya kutunza na kuzisimamia kwa pamoja.
Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dr. Richard Sezibera`amesema semina hiyo inafanyika wakati muafaka kwa kuwa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki ndio limemaliza kuandaa muswada kuhusu usimamizi wa mfumo ikolojia wa rasilimali za aina hiyo kwa nchi wanachama na kuongeza kuwa baada ya semina hiyo Sekretarieti ya jumiya ya Afrika Mashariki itapeleka wawakilishi wake kwenye mkutano wa dunia wa mazingira endelevu wakiwa na ujumbe mahususi katika kutunza mazingira.
Nae Mkurugenzi wa Sekta za Uzalishaji ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Dr. Nyamanje Weggoro amesema Semina hiyo itatoa fursa ya pekee kwa nchi wanachama wa umoja huu kujadili njia mahususi za namna ya kuziendeleza rasilimali hizo.
Kwa upande wake mwakilishi toka Wizara ya Mambo ya Afrika Mashariki kwa Tanzania, Ashili Imile amesema rasilimali zinazotumiwa kwa pamoja na nchi ambamo zinapatikana wakati mwingine zimekuwa zikisababisha migogoro baina ya nchi hizo kutokana na mfumo duni wa kusimamia rasilimali hizo ambapo madhara ya uharibifu yanapotokea huzipata nchi zote zinazotumia rasilimali husika.
Semina hiyo inafanyika kwa siku 3 na imeandaliwa kwa pamoja kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jamii ya utunzaji wanyamapori WCS kwa msaada kutoka Shirika la huduma za Misitu la Marekani USFS.
0 comments:
Post a Comment