Home » » Updates : Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha ahamia Chadema

Updates : Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha ahamia Chadema


James Ole Millya

MWENYEKITI wa UVCCM, Mkoa wa Arusha,kwa miaka mitano, James Ole Millya,ametangaza kujiuzulu nafasi zote kuanzia Taifa hadi Mkoa na kutangaza kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa madai kuwa CCM imefilisika kimawazo na haitoi matumaini kwa watanzania.

Aidha alisema hawezi kuendelea kupanda gari lenye pancha lukuki, hivyo ameamua kupanda gari lisilo na pancha na lenye kutoa matumaini mapya kwa watanzania.

Hayo ameyasema leo, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Hoteli ya Kibo Palace, iliyopo Jijini hapa.

Amesema mara nyingi alikuwa akikemea mambo ambayo yanaweza kubomoa chama cha CCM kwa upendo, lakini alikuwa akipuuzwa kwa sababu ya chama hicho kuwa na kikundi cha wenyewe.

“Mimi nanukuu maneneo ya Nyerere kuwa alishawahi kusema CCM sio mama yangu na mimi pia CCM sio mama yangu na natangaza rasmi, kuondoka ndani ya chama hiki na najiunga na Chadema, sababu ndicho chama chenye kuleta tumaini jipya kwa watanzania,”alisema.

Ametaja nafasi alizoachia ngazi ni pamoja na Mjumbe kamati ya utekelezaji UVCCM Taifa, Mjumbe kamati ya siasa Mkoa na Mjumbe Halmashauri Kuu CCM Mkoa.

Amesema kuwa inasikitisha kuona Vijana wa UVCCM Mkoa wa Pwani, wanatoa matamko kuwa Rais ajaye 2015 hatatoka kanda ya Kaskazini na anayemfahamu ni Rais peke yake ambaye ni Jakaya Kikwete.

Millya alisema cha kusikitisha pale alipokemea kauli hiyo alipuuzwa na hadi sasa Ikulu haijawahi kutoa kemeo kwa Vijana hao na wala kukataza kauli hizo kutolewa, jambo lililompa jibu kuwa Ikulu inahusika kwa namna moja au nyingine na kauli hiyo.

Aidha alisema kuna Vijana wengi walioko ndani ya CCM wakiishi kwa  matumaini ya kusubiri kuteuliwa nafasi ya Mkuu wa Wilaya kama sio Mkoa, ila yeye hawezi kuishi kw amatumaini kama muathirika wa Ukimwi.

Hata hivyo alitoa wito kwa Vijana wote wenye nia ya dhati na mapenzi mema ya nchi yao, kumfuata Chadema ambako kunatoa tumaini jipya la maisha ya watu.

Millya ambaye alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa UVCCM tangu 2008 hadi sasa, aliwashukuru vijana  kwa kumpa ridhaa hiyo na ataendelea kuwashukuru, ila ameamua kwa ridhaa yake kuachia ngazi zote kwa ajili
ya ukombozi wa kweli.

Millya hivi karibuni alijitosa kinyang’anyiro cha kugombea Ubunge wa Afrika Mashari ndani ya Chama chake cha CCM, lakini alichijiwa baharini na kutolewa jina lake.

Wakati Kiongozi huyo akitangaza kuachia ngazi hiyo ya juu ya UVCCM,ndani ya Chama cha CCM, Mkoa wa Arusha, Vijana mbalimbali wameonekana kutoamini walichosikia na wengi wao wakionyesha nia ya kumfuata.

Akizungumza kwa niaba ya vijana wenzake, Hamisi Bakari, alisema kuwa amesikitishwa na kiongozi wake kuhama chama na hiyo inaonyesha CCM imeoza na hivyo kilichobaki hata wao kumfuata anakokwenda.

“Mimi na wenzangu tutakwenda huko aliko kwa sababu kama yeye kiongozi ameamua kujiunga Chadema hata sisi wadogo hatuna mana ya kuendelea kubaki huku,”alisema.
Habari na Rosemary Kitosia,Arusha

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa