Home » » CCM, Chadema washutumiana Arumeru

CCM, Chadema washutumiana Arumeru



Mmoja wa wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kalisti Lazaro akipakiwa kwenye gari la Polisi baada ya kudaiwa kuvamia mkutano wa CCM eneo la Ngaresero, Arusha. (Picha na Marc Nkwame).
SIKU chache kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa ubunge Arumeru Mashariki, vyama vyenye ushindani mkali katika uchaguzi huo, CCM na Chadema, vimeanza kutupiana maneno. 


CCM jana ilitoa shutuma mpya kuwa Chadema inasambaza taarifa kwa wananchi kwamba mgombea wake, Sioi Sumari, amejitoa kwenye kinyang’anyiro hicho, huku wafuasi wanaodaiwa kuwa wa Chadema wakichora picha mbaya za mgombea huyo wa CCM. Chadema nao pamoja na kukana taarifa hiyo, wamedai kuwa CCM mikutano yao imejaa matusi. 



Siasa chafu Chadema Akihutubia wakazi wa kijiji cha Usa River katika mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa michezo wa Ngaresero juzi jioni, Meneja wa Kampeni za CCM, Mwigulu Nchemba alidai Chadema wameanza kufanya siasa chafu katika mikutano ya kampeni iliyofanyika juzi. 


Nchemba alidai kwamba viongozi wa Chadema wakifanya kampeni katika kijiji cha Leguruki waliwatangazia wananchi, kwamba watakuwa na kazi rahisi ya kuchagua mbunge kwa kuwa mgombea wa CCM ameshajitoa. 


“Ndugu wananchi jambo hili linadhihirisha kauli yangu, kwamba viongozi wa Chadema na hasa Dk. Slaa (Willibrod – Katibu Mkuu) wameanza kuchanganyikiwa, na muda si mrefu wataanza kuokota makopo,” alidai Nchemba. Alidai CCM ilitambua, kwamba Chadema wangeweza kufanya hivyo Jumapili kutokana na Aprili mosi kuwa Siku ya Wajinga, lakini wameamua kufanya hivyo mapema jambo ambalo alisema halikubaliki. 


“Haya ni mambo ya ajabu sana. Wanazunguka vijiji vyote na helikopta kutangaza kuwa mgombea wetu kajitoa, wanasema kajitoa lakini Sioi si huyu hapa mnamwona?” Alihoji Nchemba. 


Aliwataka wananchi kuwa macho na propaganda hizo alizosema zinatokana na Chadema kubaini kuwa watashindwa katika uchaguzi huo na hivyo kutafuta mbinu zitakazofanya wananchi kuhadaika na kumpigia kura mgombea wa Chadema, Joshua Nassari. 


Akizungumza katika mkutano huo, Sioi alisema anajivunia kugombea ubunge kutoka katika chama kinachounda Serikali kwa kuwa na utajiri wa watendaji, kuanzia Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, mawaziri, naibu mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya ambao alisema watakuwa msaada mkubwa katika utendaji wake wa kazi. 


“Ndugu wananchi juzi alikuwepo hapa Mzee Stephen Wassira, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Sera, Uratibu na Uhusiano… siku mkinichagua nitamfuata nyumbani na kukataa kutoka sebuleni hadi asikilize kilio chenu,” alisema Sioi. 


Alisema pamoja na kubuni vyanzo vya ajira kwa vijana, pia atahakikisha madereva wa bodaboda wanawezeshwa kwa kupewa vitendea kazi na mitaji itakayowawezesha kukuza biashara na kuinua biashara zao.

Habari Leo

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa