ONSPOT MAGAZINE

ONSPOT MAGAZINE

WATUHUMIWA KESI YA UGAIDI WAHOJI ALIPO MWENZAO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Watuhumiwa wa kesi ya ugaidi na kudaiwa kufanya uwakala wa kusajili vijana kujiunga kundi la Al- Shabaab la nchini Somalia wameutaka upande wa Mashitaka kuwaeleza alipo mtuhumiwa namba mbili, Abdallah Thabit.
Malalamiko hayo yaliyotolewa jana mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa ya Arusha, Rose Ngoka, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa. 

Mtuhumiwa mmoja katika kesi hiyo alinyoosha mkono na kumuomba Hakimu Ngoka auulize upande wa Mashitaka ni kwanini hadi jana wakati kesi hiyo ilipokuwa ikitajwa Thabit hakuwa amefikishwa mahakamani.

“Mheshimiwa Hakimu Julai 24, mwaka huu upande wa Mashitaka ulidai kwamba ungemleta mtuhumiwa Thabit, lakini mpaka leo (jana) hatujui ni kwanini hajaletwa mahakamani,” alisema mtuhumiwa, Ally Hamis.

Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Gaudencia Joseph, alidai kwamba ndiyo mara yake ya kwanza kusimamia taarifa hiyo, hivyo atakwenda kuifanyia kazi.

“Mheshimiwa Hakimu, taarifa hii ndiyo naisikia leo (jan) hapa, na hii ni kwa sababu Mwendesha Mashitaka anayesimamia shauri hili hayupo, hivyo sikuwa na taarifa kama walishawahi kuwasilisha malalamiko yao.

“Lakini tarehe ijayo naamini watapata taarifa za mshitakiwa mwenzao kwanini hajaletwa kama walivyodai mbele yako. Lakini pia upelelezi wa shauri hili haujakamilika, hivyo tunaomba tena tarejhe nyingine ya kutajwa,” alisema Joseph. Majibu  hayo yalionekana kutomridhisha mtuhumiwa huyo na kumuomba tena Hakimu Ngoka nafasi na kusisitiza kuwa hata Julai 24, mwaka huu majibu yaliyotolewa ni kama hayo.

Hata hivyo, Hakimu Ngoka aliingilia kati na kutoa ufafanuzi kwamba majibu sahihi yangeweza kutolewa na Mwendesha Mashitaka aliyekuwapo  kwani hata hakimu anayesikiliza shauri hilo naye hakuwapo.

“Tatizo ni kwamba hakimu na mwendesha mashitaka wote hawapo leo (jana), tunaiahirisha kesi hii hadi Septemba 3, mwaka huu,” alisema Hakimu Ngoka.

Washitakiwa  hao wameshitakiwa kwa makosa yaliyo chini ya Sheria ya kuzuia ugaidi, namba 22  ya mwaka 2002 inayosema upelelezi ukishakamilika, Mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kuisikiliza na kutoa uamuzi

Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka ya kuua, kujaribu kuua, kusajili na kusafirisha vijana kujiunga na Al-Shabaab.
Pia, wanahusishwa na  tukio la  mlipuko wa bomu katika baa ya Arusha Night Park jijini Arusha na kusababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi wengine 16.

Washitakiwa hao ni Abdallah Athumani, Abdallah Thabit, Ally Hamisi, Abdallah Wambura, Rajabu Hemed, Hassan Said, Ally Hamisi, Yasini Sanga, Shaabani Wawa, Swalehe Hamisi, Abdallah Yasini, Abdallah Maginga na Sudi Nasibu Lusuma.

Wengine walioongezwa katika kesi hiyo ni Shaban Musa, Athuman Hussein, Mohamed Nuru, Jafari Lema, Abdul Mohamed na Said Michael Temba.
 
CHANZO: NIPASHE

MADIWANI WAMTAKA MKURUGENZI LONGIDO KUSITISHA MRADI WA MAJI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Baraza la Madiwani wa Halmshauri ya Longido, limetoa tamko kutokana na mgogoro wa mipaka kati ya Wilaya za Longido na Arumeru kwa kumtaka Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Julius Chalya, kusitisha ujenzi wa  mradi wa maji ambao mpaka sasa umegharimu Sh. milioni 200.
Akizungumza katika Baraza la Madiwani lililofanyika katika halmashauri hiyo mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Joseph Ole Sadira, alisema wameamua kutoa tamko hilo kutokana na Halmashauri kuweka alama za mipaka mara tatu mfululizo na alama hizo kutolewa bila mtu yeyote kuchukuliwa sheria.

Hata hivyo, madiwani hao walisema chanzo cha mradi huo kipo wilayani Arumeru, hivyo wana shaka ya kutumia fedha nyingi za wananchi katika kuhakikisha wananchi wa Longido wanapata maji.

“Baraza hili limeamua kutoa tamko kuwa walioshiriki kung'oa alama za mipaka wabainishwe na wachukuliwe hatua za kisheria, gharama zilizotumika katika uwekaji wa alama za mipaka zirudishwe na tunaomba Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi isaidie kutatua migogoro ya mipaka,” alisema Sadira.

Akisoma taarifa ya mgogoro wa mipaka ya Wilaya za Longido, Arumeru na Monduli, Mkuu wa Idara ya Ardhi, Maliasili na Mazingira wilayani Longido, Elia Samson, alisema juhudi zilizofanywa na kamati mbalimbali na za halmashauri hiyo kuweka alama mara tatu, bado zimeshindwa kudumu na alama hizo kung’olewa mara baada ya kuwekwa hazijazaa matunda.

“Mei 28, mwaka huu, Kamati ya Ulinzi na Usalama za Wilaya ya Longido, Arumeru na Monduli, ziliagiza wataalam waendelee kurudisha alama husika ambapo jumla ya Shilingi milioni 3.6 zimetumika kama zilivyoagizwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha na kazi ilianza Juni 2, mwaka huu ambapo alama hizo ziling’olewa tena kwa mara ya pili na Mkuu wa Mkoa akaagiza kurejeshwa tena,” alisema Samson.

Hata hivyo, alisema kuanzia Juni 17, mwaka huu hadi Juni 19, mwaka huu, kazi ya urejeshwaji alama hizo ulifanyika lakini Juni 19, mwaka huu majira ya jioni, alama husika ziling’olewa tena na zoezi hilo limesitishwa mpaka sasa kwa sababu za kiusalama kwa wapimaji.

Baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo akiwamo Diwani wa kata ya Longido, Motika Kasosi, wamelaani watu wanaong’oa alama hizo na mpaka sasa hawajachukuliwa hatua yoyote huku halmashauri hiyo ikipoteza fedha za walipa kodi na kusababisha hofu ya kutokamilika kwa mradi mkubwa wa maji.

Kasosi alisema suala hilo la mipaka siyo la kufumbiwa macho kwa kuwa halmashauri hiyo inaweza kutekeleza mradi huo mkubwa wa maji na maji hayo yasiwafikie wananchi wa Longido na hivyo serikali kupoteza bure fedha za walipa kodi.

Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Esupat Ngulupa, ameomba serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kuingilia kati mgogoro huo kutokana na hatua zilizochukuliwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama kutozaa matunda.
CHANZO: NIPASHE

TEMBO WAVAMIA MAKAZI, WAUA, KUJERUHI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mkuu wa Wilaya ya Longido, James Ole Millya
 
Kundi la tembo limevamia makazi ya wananchi wa Kata ya Tingatinga, Wilaya ya Longido, mkoani Arusha na kusababisha kifo cha mtu mmoja na mwingine kujeruhiwa.
Katika hekaheka ya kukabiliana na tukio hilo, tembo mmoja ameuawa kwa ushirikiano wa wananchi na askari wa wanyamapori kutoka Kikosi cha Kuzuia Ujangili Kanda ya Kaskazini.

Wananchi wa kata hiyo, waliliambia NIPASHE kuwa aliyeuawa na tembo hao ni mtoto  wa miaka tisa aliyetajwa kwa jina la Fred Joseph, huku Paulo Lukari, akijeruhiwa na kulazwa hospitali. 

Wakizungumza baada ya Kikosi cha Kuzuia Ujangili Kanda ya Kaskazini kufika na  kushirikiana nao kumuua tembo aliyesababisha madhara hayo, wananchi hao  wamelalamikia watendaji wa sekta ya wanyamapori kwa kuendelea kukaa mijini na  kusubiri kupewa taarifa wakati wananchi vijijini wakiendelea kuuawa.

Diwani wa Kata ya Tingatinga, Sabore Olemoloimet, ameiomba serikali kuhakikisha  watendaji wanaoshughulikia migogoro ya wananchi na wanyamapori kuhamia maeneo  husika ili wawadhibiti wanyama kabla hawajaleta madhara.

“Kuna haja ya watendaji wa sekta hii kuwa karibu na wananchi, hasa kwenye maeneo hayo, ambayo yamekuwa yakilalamikiwa kila siku na wananchi, kwani pamoja na umuhimu wa wanyamapori tatizo hili linawaongezea wananchi umaskini,” alisema Sabore Olemoloimet, ambaye ni Diwani Kata ya Tingatinga.

Mkuu wa Wilaya ya Longido, James Ole Millya, alithibitisha kuwapo kwa udhaifu mkubwa kwa watendaji wanaoshughulikia wanyamapori na kwamba, licha ya kutoa  maelekezo mara kadhaa bado hayafanyiwi kazi.

“Nimeshamwandikia mkurugenzi barua, lakini naona bado hajachukua hatua. Itabidi nichukue hatua zaidi kwa ngazi za juu,” alisema Millya. 
Baada ya tembo huyo kuuawa, makundi ya wananchi wa eneo hilo yalifika na kuanza  kugawana kitoweo, huku wakimshukuru Mungu kwa kuwawezesha kuondokana na tatizo hilo na pia kupata kitoweo.

Baadhi walitaka wapewe kipaumbele kwa kupewa nyama nyingi kwa madai kuwa wameathirika zaidi na wanyama hao. 

Vilio vya wananchi juu ya madhara yanayosababishwa na wanyamapori, wakiwamo  tembo vimekuwa vikisikika katika kona mbalimbali nchini jambo linaloonyesha kuwa  bado tatizo hilo halijapata ufumbuzi wa kudumu.
CHANZO: NIPASHE

WATUHUMIWA WA MABOMU ARUSHA MAHAKAMANI TENA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Watuhumiwa 19 wanaotuhumiwa kulipua bomu kwenye viwanja vya Soweto, wamepandishwa kizimbani kwa mara ya pili mbele ya hakimu Hawa Mguruta na hawakutakiwa kujibu chochote.
Washitakiwa hao waliomba mahakama iwaruhusu kuonana na ndugu zao, ili wawape maagizo ya kifamilia.

Aidha, walidai mtuhumiwa mmoja ni mgonjwa na daktari alimpa maagizo ya kula aina maalum ya chakula, ila tangu apelekwe gerezani hapati chakula zaidi ya mchicha mchemsho na maharage, hali inayosababisha wakati mwingine kupoteza fahamu.

Hakimu Mguruta akijibu hoja hizo, alisema suala la ndugu zao kwenda mahakamani kuwaangalia lipo juu ya uwezo ila wanaweza kufuata taratibu za magereza kwa kuandika barua na kuomba kama itawezekana.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Agosti 29 mwaka huu, itakapotajwa tena.

Awali  Mawakili wa serikali waliwasomea mashitaka yao kwa kupokezana ambao ni Augustino Kombe, Marcelino Mwamunyange na Felix Kwetukia, walidai mahakamani hapo, washitakiwa hao wanashitakiwa kwa kula njama ya kufanya ugaidi, kufadhili kufanyika kwa ugaidi.

Makosa mengine ni kufanya mauaji baada ya kutupa bomu, kusababisha majeraha, kutoa ushirikiano kufanyika kwa ugaidi, kukusanya dhana ili kutenda ugaidi na kusambaza dhana ili kutenda ugaidi.

Walidai kuwa washitakiwa hao wanadaiwa kufanya makosa hayo Julai 3 mwaka huu, Juni 15, kwenye viwanja vya Soweto, katika mkutano wa Chadema na kusababisha mauaji na majeraha kwa watu. Pia walidai kuwa washitakiwa hao Juni 23, 24 na Julai 21 mwaka huu, walikusanya mabomu saba ya kurusha kwa mkono kwa lengo la kuwezesha kufanyika kwa ugaidi.

SOURCE: NIPASHE

ARUSHA MERU YAKOPESHA AKINAMAMA MILIONI 151/-

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 

ZAIDI ya mikopo ya sh. milioni 151 imetolewa kwa akinamama 287 kwa muda wa miaka mitatu tangu mwaka 2012 hadi 2014 na kikundi cha Arusha Meru Women Saccos lengo ikiwa ni kuwainua akinama kuichumi.

Hayo yalisemwa na mwenyekiti wa kikundi hicho Bi.Eva Kaaya juzi katika maonyesho ya Nanenane katika Viwanja vya Themi jijini Arusha.

Alisema kuwa hadi sasa wametoa mikopo kwa akinamama zaidi ya sh.milioni 151 kwa ufadhili wa Canadian Co-operative Association kupitia Moshi University College of Co-operative and Business Studies.

Alisema kuwa lengo lao hasa la kufanya hivyo ni kuwainua akinamama kiuchumi hali itakayopelekea wao kuondokana na umaskini katika familia zao huku akiweka wazi kuwa hadi sasa mikopo iliyorejeshwa ni sh. milioni 97,644,066 na mikopo iliyobaki ni sh.milioni 53,735,934.

Bi.Kaaya alisema kuwa wamekuwa wakiwahudumia akinamama kutoka Arusha na Arumeru kwa kuwapa mikopo wajasiriamali, ambapo sharti la kupata mkopo ni lazima awe na hisa katika kikundi hicho na kumfanya mwombaji wa mkopo awe mmiliki halali wa Saccos.

"Ili akinamama wapate mkopo ni lazima wawe katika kikundi cha watu watano,awe mwanachama hai na awe na akiba kwa kufuata masharti hayo mwombaji anapewa mkopo bila ya msharti magumu," alisema Bi.Kaaya.

Kwa upande wake katibu wa kikundi hicho Bi. Martha Temba alisema kuwa njia mojawapo iliyowafanya wakafika hapo ni utoaji wa mafunzo kwa akinamama juu ya elimu ya Saccos kwa kuweka na kukopa inayotolewa na Chuo cha Ushirika Moshi.

"Mafanikio tuliyonayo sasa ni kutokana na akinamama kupewa elimu ya Saccos,kabla ya elimu walikuwa wakichukua mikopo kienyeji hali iliyopelekea wengine kushindwa kuendelea na kikundi," alisema Bi.Temba.

Aidha, alisema kuwa wapo na timu kutoka ushirika ambapo wanawafikia kina mama katika kata na vijijini na kuwapa elimu ya Saccos.

Naye Afisa Ushirika Halmashauri Wilaya ya Arusha DC Bi.Sophia Shoko alisema kuwa majukumu yao makubwa ni kusimamia sheria na kukagua,kuhamasisha wanachama kujiunga katika Saccos.

Pia aliongeza kuwa kazi yao ni pamoja na utoaji elimu ya ushirika, utunzaji wa kumbukumbu,haki na wajibu wa mwanachama,huku akiwataka akinamama kupunguza kuwa na mikopo mingi isiyokuwa na tija

Chanzo:Majira

PINDA APONGEZA SEKTA YA UTALII ARUSHA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ameimwagia sifa hoteli maarufu ya Ngurdoto yenye hadhi ya nyota tano, iliyopo nje kidogo ya jiji la Arusha, kutokana na kuwa na ukumbi mkubwa wa kisasa wenye uwezo wa kuketisha watu zaidi ya 3,000 kwa wakati mmoja na kueleza kuwa ukumbi huo ni mkombozi kwa sekta ya utalii nchini.

Aidha alikitaka kituo cha kimataifa cha mikutano cha Arusha, AICC kuboresha kumbi zake ili ziendane na wakati huku akitahadharisha kwamba upo uwezekano wa kituo hicho kukosa mikutano iwapo kitashindwa kuboresha kumbi zake ziwe na hadhi ya kimataifa.

Kauli hiyo ameitoa jijini hapa wakati akifungua mkutano wa wadau wa maji unaofanyika katika ukumbi huo huku akitumia muda mwingi kutazama mandhari ya ukumbi huo.

"Kwa kweli hili jengo ni la kisasa sana nimetembea sehemu nyingi hapa nchini sijawahi kuona ukumbi wa kisasa kama huu, kwa kweli Mrema (mmiliki wa hoteli) ametuokoa sana, hii ni changamoto kwa AICC wajitahidi kuboresha kumbi zao vinginevyo watapigwa mweleka,"alisema Bw.Pinda.

Pinda aliongeza kuwa Tanzania kuwa na ukumbi wa kisasa kama huo ni heshima kwa taifa na hivyo serikali itajitahidi kuleta mikutano ya kutosha.

Awali mkuu wa mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, alimweleza Waziri Mkuu Pinda kwa kuitaka serikali iangalie uwezekano wa kuhamishia mikutano mingi mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kufanyika jijini hapa kwa kuwa tayari inao vigezo vyote vya kufanikisha mikutano hiyo.

Bw.Mulongo alisema ni bora mikoa mingine ikakubali kuuachia mkoa wa Arusha kuandaa mikutano mbalimbali kutokana na vigezo vilivyopo zikiwemo hoteli nyingi zenye kumbi za kisasa, huku akitolea mfano ukumbi huo wa Ngurdoto maarufu kwa jina la Tanzania Convention Center.

"Karibuni sana Arusha yale mambo yetu ya zamani tumeshaacha na wale wanaoamini wangekutana na mabomu sasa hayapo tena, karibuni kwenye ukumbi mpya wa kisasa zaidi, mheshimiwa waziri mkuu lazima mikoa mingine wakubali kuuachia mkoa wa Arusha kuandaa mikutano mbalimbali kwa sababu vigezo vyote tunavyo,"alisema Bw.Mulongo.

Aidha alisema mkoa wa Arusha ni kituo cha utalii na vivutio vingi vya kumfanya mgeni afurahie mandhari yaliyopo hivyo aliongeza kwa kuwataka wadau mbalimbali kuwa hakuna haja ya kupeleke mikutano sehemu nyingine

Chanzo:Majira

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa