WAKILI maarufu jijini Arusha, Mediam Mwale na wenzake watatu jana
walisomewa mashitaka 42 kwa mara ya nne katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Mkoa wa Arusha.
Mwale anayemiliki Kampuni ya Uwakili ya JJ Mwale Advocates na wenzake
watatu, awali walisomewa mashitaka mapya 44 ya utakatishaji fedha
haramu, kula njama na kughushi baadhi ya nyaraka na kujipatia kiasi cha
cha dola za Marekani milioni 18 sawa na zaidi ya Sh bilioni 40. Lakini
jana walisomewa mashitaka 42 mbele ya Hakimu Mkazi, Nestory Baro baada
ya kesi hiyo kuondolewa Mahakama Kuu juzi na washitakiwa kukamatwa tena.
Mbali ya Mwale, wengine walioshitakiwa ni Meneja wa Benki ya CRDB
tawi la Mapato jijini Arusha, Boniface Thomas, mfanyabiashara wa jijini
Nairobi, Kenya, DonBosco Gichana “Bob James Onderi” na Elias Ndejembi.
Akiwasomea mashitaka kwa nyakati tofauti, Mwendesha Mashitaka wa
Serikali, Shedrack Kimani na Oswald Tibabyakyoma, walidai kuwa kwa
nyakati tofauti kati ya mwaka 2010 na 2011 washitakiwa hao walitenda
makosa hayo na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Hata hivyo, Mwale na wenzake walikana mashitaka hayo na kuiomba
mahakama kuieleza Jamhuri kuacha danadana katika kesi hiyo na katika
mambo ya kisheria, kwani mahakama za juu zilishaifuta kesi kwa zaidi ya
mara tatu, lakini Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) amekuwa akiiondoa na
kuirudisha tena kwa makosa yale yale.
“Mheshimiwa hakimu kesi hii imefutwa mara tatu na Mahakama Kuu na
jana (juzi) Jaji David Mrango aliungana na DPP kuiondoa kesi hii, lakini
alionya kuacha kuirudisha tena kwani watuhumiwa wamekaa rumande kwa
zaidi ya miaka sita hivyo watende haki,” alidai Mwale.
Baada ya hali hiyo, Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Tibabyakyoma
alidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na aliomba tarehe ya kuanza
kusikilizwa. Hakimu Baro alisema kesi hiyo itaanza kusikilizwa kesho na
mawakili wa utetezi na wa Serikali walitakiwa kujiandaa kwani kesi hiyo
itasikilizwa mwezi mzima. Mwale na wenzake wanatetewa na mawakili Albert
Msando, Innocent Mwanga, Julieth Tarimo na Omary Omary na Mawakili wa
Serikali mbali ya Tibabyakoma, ni Pius Hilla na Shedrack Kimani.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment