JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
TAARIFA KWA UMMA
ZOEZI
LA KUONDOA MIFUGO NA MAKAZI NDANI YA HIFADHI YA TAIFA SERENGETI NA KWENYE MPAKA
WA PORI TENGEFU LOLIONDO
Kamati
ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ngorongoro, kwa kushirikisha Hifadhi ya Taifa
Serengeti na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, inaendesha zoezi la kuondoa
mifugo na makazi ndani ya hifadhi ya Taifa Serengeti na kwenye mpaka wa Pori
Tengefu Loliondo.
Zoezi
hilo lililoanza tarehe 10 Agosti 2017 litadumu kwa siku kumi na nne na linashirikisha
Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Ngorongoro, Jeshi la Polisi, Usalama wa
Taifa, Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Hifadhi ya Taifa Serengeti na Hifadhi
ya eneo la Ngorongoro.
Zoezi
hilo linalenga kunusuru uhifadhi ndani ya hifadhi, ndani ya Pori Tengefu
Loliondo, na ndani ya mfumo ikolojia wa Serengeti na pia kunusuru utalii katika
mfumo ikolojia huo.
Aidha,
hatua hii ya kuondoa makazi na mifugo kutoka katika maeneo ya mipaka ya Pori
Tengefu Loliondo kutaongeza uhakika wa kupatikana malisho ya mifugo wakati wa
kiangazi kwa kuwa hakutakuwepo na makazi ndani ya Hifadhi na ufugaji holela.
kimsingi
zoezi hili linaendana na wito wa Serikali wa kuondoa mifugo ndani ya maeneo
yote yaliyohifadhiwa nchini.
Katika
kutekeleza zoezi hili, Mkuu wa Wilaya
Ngorongoro, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama
Wilaya ya Ngorongoro Bwana Rashidi Taka, alitoa maelekezo yafuatayo:
1. Zoezi
litafanyika ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti na kwenye mpaka wa Pori Tengefu
Loliondo. Kwa upande wa mpaka wa Pori Tengefu Loliondo zoezi litaanzia
kaskazini hadi kusini urefu wa kilometa 90, na upana wake utakuwa kilometa 5.
Kwa ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti litafanyika upande wa mashariki kuanzia
milima ya Kuka (kaskazini) hadi kigingi na. SNP 9 (kusini);
2. Maboma
yatakayokutwa ndani ya hifadhi yatateketezwa kwa moto na watu watakaokutwa na
mifugo watachukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kupelekwa mahakamani;
3. Maboma
yaliyoko ndani ya mpaka wa Pori Tengefu Loliondo - kwenye mpaka na ndani ya kilometa tano -
wataondolewa ili warudi vijijini. Eneo hilo litabaki kwa ajili ya malisho na si
kwa ajili ya makazi. Uwepo wa makazi
kwenye mpaka wa Hifadhi ya Taifa Serengeti umekuwa kichocheo kikubwa cha mifugo
kuingizwa hifadhini.
Zoezi
hili linalenga kuondoa changamoto kubwa ya mifugo kuingizwa Hifadhi ya Taifa
Serengeti na kwenye mpaka wa Pori Tengefu Loliondo, kupambana na uvamizi mkubwa
uliofanywa na wahamiaji haramu kutoka nchi jirani na kunusuru vyanzo vya maji
kutokana na mifugo kulishwa kwenye vyanzo vya maji na hivyo kusababisha vyanzo
hivyo kuharibika na kukosekana kwa maji kwa ajili ya mifugo na wanyamapori.
Hadi
sasa zoezi hili la kuondoa mifugo na makazi ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti
na kwenye mpaka wa Pori Tengefu Loliondo linaendelea vizuri likihusisha kuchoma
moto maboma yote yaliyoachwa na wafugaji walioondoka wakati wa zoezi.
Wizara
ya Maliasili na Utalii inapenda kuufahamisha umma kuwa hakuna watu wanaopigwa
katika zoezi hili.
Pia,
Wizara ya Maliasili na Utalii inapenda kuutaarifu umma kuwa habari
zinazosambazwa mitandaoni ni upotoshaji wa ukweli wenye nia ovu ya kujenga
chuki dhidi ya Serikali kwa wananchi wa Loliondo
na maeneo yanayopitiwa na zoezi hilo.
Aidha, Wizara ya Maliasili
na Utalii, inapenda kuweka bayana kuwa, taarifa za kupigwa risasi Pormoson Losso
mwenye umri wa miaka 23, mkazi wa Ololosokwan zilitolewa tarehe 8 Agosti 2017
na hazihusiani na zoezi tajwa kwani tukio hilo
lilitokea siku tano kabla ya kuanza zoezi la kuondoa mifugo na makazi
ndani ya hifadhi wakati zoezi hili lilianza
kutekelezwa Jumapili tarehe 13 Agosti 2017.
Hata
hivyo Serikali inawapongeza wananchi wengi miongoni mwa wafugaji kwa kuunga
mkono zoezi hili na kwa ushirikiano wanaotoa.
Serikali
inatoa onyo kwa yeyote anayejihusisha na upotoshaji wa ukweli kuhusu zoezi hili
lenye nia njema linalolenga kunusuru hifadhi, kuacha mara moja ili kujiepusha
na hatua za kisheria zitakazochukuliwa pindi atakapobainika.
Imetolewa
na;
Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini
17/08/2017
0 comments:
Post a Comment