Imeandikwa na John Mhala, Arusha
MSHITAKIWA wa kwanza katika kesi inayowakabili washitakiwa 15
wakiwemo 13 waliokuwa wafanyakazi wa Benki ya Exim (T) Tawi la Arusha,
Bimel Gondael (37), ameiambia mahakama kuwa mashahidi 37 wa jamhuri
waliotoa ushahidi katika mahakama hiyo hakuna aliyesema yeye aliharibu
nyaraka za benki hiyo.
Gondael ambaye ni Mtanzania mwenye asili ya Kiasia na alikuwa meneja
mzoefu katika benki hiyo tangu 2009 hadi 2012, alidai hayo wakati
akiongozwa na wakili wake, Adam Jabir mbele ya Hakimu Mfawidhi wa
Mahakama ya Wilaya ya Arusha/Arumeru, Deusdedit Kamugisha. Gondael
ambaye ni shahidi wa 15 wa upande wa utetezi, alidai kutokana na
mashahidi wa jamhuri kutomtaja kuhusika na shitaka hilo, aliomba
mahakama kumwachia huru.
Alidai Benki ya Exim haikuwahi kutoa taarifa kuwa ilipata hasara
kutokana na wizi uliotokea mwaka 2012 na hakuna shahidi wa benki hiyo
aliyesimama katika mahakama hiyo kueleza kuwa benki ilipata hasara au
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) nayo ilipata hasara kutokana na
wizi huo.
“Lazima kuwe na taarifa ya kifedha ya kila mwaka ya kuonesha hasara
na faida na katika kesi hii lazima taarifa hiyo ya ukaguzi wa ndani au
nje ingeletwa hapa mahakamani kuthibitisha hilo lakini halikufanyika.
Shitaka hili siyo la kweli dhidi yangu na hakuna shahidi aliyethibitisha
kuwa niliharibu nyaraka za Benki ya Exim, hivyo naomba mahakama niachie
huru,” alidai Gondael.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment