Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe ameeleza jinsi mamilioni ya fedha
yatakavyotumika kugharimia uchaguzi mdogo katika kata nane za mikoa ya
Arusha na Kilimanjaro kuziba nafasi zilizoachwa wazi na madiwani wa
Chadema waliojiuzuru.
Akizungumza
katika mikutano tofauti ya hadhara jimboni kwake, Mbowe ambaye pia ni
mbunge wa Hai, alisema uchaguzi mdogo katika kata moja unatarajia
kugharimu Sh250 milioni.
Katika
majimbo ya Arusha Mjini na Arumeru Mashariki mkoani Arusha na Hai
mkoani Kilimanjaro ambayo yote yako chini ya Chadema, jumla ya madiwani
nane walijiuzulu, wakisema wanamuunga mkono Rais John Magufuli.
Endapo
makadirio ya Mbowe yatakuwa ni sahihi, kiasi cha Sh2 bilioni kitatumika
kufanya uchaguzi mdogo katika kata tatu za jimbo la Hai, nne za jimbo
la Arumeru Mashariki na moja ya Arusha.
Alipoulizwa
kuhusu gharama hizo, mkurugenzi wa uchaguzi wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi(NEC), Kailima Kombwey alisema “huwa sipendi ku-comment
wanaposema wanasiasa sababu I’m not a politician (mimi si mwanasiasa)”.
Akizungumza
katika mikutano tofauti ya hadhara jimboni kwake kwa siku nane
mfululizo, Mbowe alisema matumizi hayo ya mamilioni ya fedha ni mabaya
kwa kuwa ni fedha za walipakodi.
Alisema
mwaka 2015 wakazi wa Mnadani walimchagua Ernest Kimath kuwa diwani wao,
lakini akasema ni jambo la aibu kwamba CCM na viongozi wa serikali
wilayani Hai wamerubuni watu.
“Haya
ni matumizi mabaya ya fedha za umma kwa sababu gharama za kurudia
uchaguzi hapa Kata ya Mnadani pekee ni Sh250 milioni. Hizi zingeweza
kwenda kujenga shule na zahanati,” alisema.
“Serikali
inaona kuliko kuwe na diwani wa upinzani, bora turudie uchaguzi kwa
gharama ya mamilioni. Nataka niwaambie nitalala hapa Shirinjoro
tukirudia uchaguzi na haiendi popote,” alisema.
Mbowe
alisema sababu zilizotolewa na madiwani hao za kujiuzulu si za kweli,
akidai kuwa baadhi ya madiwani hao waliandikiwa barua za kujiuzulu.
Katibu
wa Chadema wa Kanda ya Kaskazini, Aman Golugwa amekuwa akisisitiza kuwa
madiwani wanaojiuzulu wanafanya hivyo kwa kushawishiwa kifedha na vyeo,
madai ambayo wameyakanusha.
Hata
hivyo CCM inadai mbinu mpya za kimkakati kulingana na kasi ya dunia na
mahitaji ya jamii, ndizo zinazowarudisha katika chama hicho.
Kauli
hiyo ilitolewa mwezi uliopita na katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM
anayehusika na siasa na uhusiano wa kimataifa, Kanali Ngemela Lubinga
wakati akizungumza na wanahabari mjini Moshi.
Kanali
Lubinga alisema hata madiwani wa Chadema katika Jimbo la Arumeru
waliojiuzulu na kumuunga mkono Rais Magufuli ni kutokana na kuridhishwa
na utendaji kazi wa Serikali.
“Hii
sasa hivi ni CCM mpya na Tanzania mpya. CCM tulijifanyia tathmini ya
miaka 40 na kuona mapungufu na tumeyarekebisha ndani ya CCM na
serikalini. Kasi hii inawavutia wengi,” alisema.
“Tumeanzisha
mbinu mpya za kimkakati kulingana na hitaji la jamii. Dunia inakwenda
spidi na spidi ya dunia inavyokwenda lazima chama tawala kiendane na
spidi hiyo na hitaji la jamii,” alisisitiza.
Katibu
wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amekaririwa akisema
anayo orodha ya viongozi wengi wa upinzani wanaoomba kurudi CCM, lakini
aliwataka wasubiri kwanza.
Arusha
na Kilimanjaro ni kati ya maeneo ambayo ni ngome kuu ya upinzani, hasa
Chadema ambayo imekuwa ikikosa upinzani kutoka vyama vingine.
Mwaka
2015, aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa aliihama CCM na kujiunga na
Chadema, akikufuatiwa na madiwani kadhaa kutoka CCM.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment