Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi la Polisi mkoani hapa limetoa onyo kwa wamiliki wa mabasi ambayo yanavunja sheria za usalama barabarani. Akizungumza na
waandishi wa habari leo mchana ofisini kwake wakati akitoa taarifa ya
matokeo ya ukaguzi wa mabasi ya abiria uliofanyika kwa siku tatu
mfululizo kuanzia tarehe 22 mwezi huu hadi 24, Kamamda wa Polisi Mkoa wa
Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo alisema
kwamba, wamiliki wa magari wanatakiwa wahakikishe mabasi yao
yanazingatia ubora unaokubalika hali ambayo itasaidia abiria wanasafiri
salama.
“Mbali
na ubora wa gari lakini pia madereva wanatakiwa wazingatie sheria za
usalama barabarani kama vile kuendesha kwa kufuata maelekezo ya alama“.
Alisema Kamanda Mkumbo.
Alisema
katika ukaguzi huo wa kushtukiza uliojumuisha mabasi yaliyokuwa
yanakwenda mikoani na yale yaliyokuwa yanaingia jijini hapa, jumla ya
mabasi 77 yalikamatwa kwa makosa ya ubovu na mwendokasi.
“Kati
ya hayo mabasi 25 yalikamatwa kwa makosa ya mwendokasi ambapo 20 kati
yao yalilipiwa tozo na matano wahusika walipelekwa mahakamani, wakati
mabasi 52 yalikutwa na makosa ya ubovu ambapo 41 yalitozwa tozo na
mabasi 11 toka makampuni mbalimbali tumeyasitishia kutoa huduma mpaka
hapo yatakapofanyiwa marekebisho”. Alifafanua Kamanda Mkumbo.
Kamanda
Mkumbo alisema kwamba pamoja na ukaguzi wa magari hayo ambao unafanywa
kila siku lakini Jeshi hilo litaendelea kufanya kaguzi za kushtukiza
mara kwa mara ili kuhakikisha abiria wa mabasi hayo wanasafiri salama,
huku akitoa wito kwa abiria watoe taarifa popote wanapogundua dereva
anakwenda kinyume na sheria za usalama barabarani.
0 comments:
Post a Comment