Home » » Mollel wa Gel awafunda wahitimu

Mollel wa Gel awafunda wahitimu

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Na Mwandishi wetu, Arusha

WAHITIMU wa sekondari nchini wametakiwa kuwa waangalifu katika uchaguzi
wa fani za kusomea kwa kusomea vitu ambavyo kweli vitakuwa na tija kwao
na taifa kwa ujumla.

Hayo yameelezwa hivi karibuni na Mkurugenzi wa kampuni ya Global
Education Link, Abdulmalik Mollel wakati alipokuwa akizungumza katika
sherehe ya kuwaaga wahitimu wa kidato cha sita wa Sekondari ya Arusha.

Alisema kuna wengi ambao wamekuwa wakisomea fani bila kujitafakari kwa
umakini kwanini ameamua kusomea fani hiyo, na hii ni kwa sababu wengine
wanafanya kwa sababu ya kuiga wengine au kutojua.

“Ukimuuliza mwanafunzi unataka ukihitimu sekondari uwe nani, anakujibu
nataka kuwa daktari, nataka kusomea biashara, nataka kusomea sheria na
kadhalika, lakini udaktari uko wa namna nyingi kwa mfano kuna madaktari
wa mifumo ya ufahamu na kadhalika.

“Hata katika biashara,mtu anaposema anataka kusomea biashara,
imegawanyika katika makundi mengi, inaweza kuwa ni biashara kwa maana ya
rasilimali watu, inaweza kuwa ni biashara kwa maana ya masoko na
kadhalika,” alisema Mollel na kufafanua kuwa kabla ya kuamua usomee nini
ni muhimu kutafuta uelewa mpana kuhusiana na mambo unayotaka kusomea.

Akizungumzia kwa upande wa kampuni yake ni kwa namna gani inawasaidia
wahitimu katika kuwa na uchaguzi sahihi wa fani, alisema kinachofanyika
katika ofisi yake ni kutoa mwongozo juu ya jambo hili.

“Tunachokifanya ni kutoa mwongozo wa mambo ya kusomea (career guidance).
Tunazo ofisi Zanzibar, Dodoma, Arusha, Mbeya na Dar es Salaam, mojawapo
ya majukumu yetu ni kutoa mwongozo juu ya uchaguzi wa fani, lakini pia
kwa wale wanaotaka kusoma nje ya Tanzania, tunawaunganisha na vyuo vya
nchi mbalimbali zikiwamo vya Marekani, Malaysia, China, India,
Uingereza, Uturuki, Afrika Kusini na kadhalika,” alifafanua Mollel.

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa