Arusha
Home » » MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA YAZIDI KUSHIKA KASI

MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA YAZIDI KUSHIKA KASI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MKU1
Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
MKU2
Askari Polisi wakiwa wananyofoa mimea ya bhangi ambayo ilikuwa imepandwa kwenye moja ya shamba lililopo katika kijiji cha Kismiri Juu kata ya Uwiro tarafa ya King’ori wilayani Arumeru. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
MKU3
Askari wa Jeshi la Polisi wakiteketeza magunia ya bhangi kwa kuchoma moto mara baada ya kuyakusanya kutoka kwenye moja ya nyumba ya mkulima wa zao hilo haramu eneo la kismiri Juu wilayani Arumeru. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
MKU4
Askari wa Jeshi la Polisi wakitoa magunia ya bhangi katika moja ya nyumba iliyopo katika kijiji cha Engalaon kata ya Mwandeti tarafa ya Muklati wilayani Arumeru mara baada ya wenyeji kukimbia na kuacha mlango. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
……………………………………………………………
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Pamoja na Jeshi la Polisi mkoani hapa kufanikiwa kuongeza takwimu za ukamataji wa madawa ya kulevya kwa makosa 75 zaidi kwa mwaka 2016 kulinganisha na mwaka 2015,imeonekana kwamba mwaka huu  2017 kwa kushirikiana  na vyombo vingine vya Usalama pamoja na Tume ya Kuratibu na Kudhibiti dawa za kulevya nchini, kasi hiyo ya kuthibiti kilimo cha madawa ya kulevya aina ya bhangi ambacho kinalimwa baadhi ya maeneo ya wilaya ya Arumeru imeanza mapema.
 
Akizungumza na waandishi wa habari ofisi kwake mara baada ya operesheni ya kutokomeza madawa hayo kufanyika kwa siku mbili, Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo alisema kwamba  Jeshi hilo pamoja na vyombo vingine limeamua kuanza kuharibu mimea iliyopo mashambani mapema hasa kipindi hiki cha masika ambapo uoteshaji ufanyika ili kazi ya kudhibiti madawa hayo huko mbeleni iwe rahisi.
 
Kamanda Mkumbo alisema katika operesheni hiyo jumla ya hekari 31 za mimea ya bhangi ziliharibiwa huku gunia 58 na kilogramu 210 ziliteketezwa kwa moto katika maeneo ya kijiji cha Kismiri Juu kata ya Uwiro tarafa ya King’ori na katika kijiji cha Engalaon kata ya Mwandeti tarafa ya Muklati wilayani Arumeru.
 
“Siku ya kwanza Jumanne tarehe 10.01.2017 Operesheni hiyo ilifanyika katika kijiji cha Kismiri Juu kata ya Uwiro tarafa ya King’ori na kupata jumla ya magunia 31 ya bhangi na kilogramu 210 za mbegu zilipatikana huku hekari 19 za mimea hiyo ziliharibiwa”.
 
“Siku ya tarehe 12.01.2017 Alhamisi operesheni hiyo iliendelea tena katika maeneo ya kijiji cha Engalaon kata ya Mwandeti tarafa ya Muklati na kufanikiwa kupatikana kwa magunia 27 na kuharibu hekari 12 za mimea ya bhangi hivyo kufanya jumla ya magunia 58 kupatikana, mbegu kilogramu 210 kupatikana na hekari 31 za mimea huo kuharibiwa”. Alifafanua Kamanda Mkumbo.
 
Kamanda Mkumbo alitoa onyo kali kwa viongozi wanaoishi au kufanyia kazi maeneo hayo, kuacha mara moja kuwaunga mkono wakulima wa bhangi.
 
Jeshi la Polisi mkoani hapa linawaonya viongozi wa maeneo ambayo zao hilo linalimwa kuacha mara moja kuwaunga mkono wakulima hao, naamini ulimaji mpaka uuzaji wa bhangi unafanywa kwa uwazi katika maeneo hayo bila wao kuchukua hatua”.
 
“Watambue kwamba wao ni walinzi wa amani katika maeneo yao na washirikiane na Jeshi la Polisi katika kutokomeza kabisa kilimo hicho cha bhangi ambayo inaleta madhara makubwa kwa jamii hasa kundi la vijana”. Alisisitiza Kamanda Mkumbo.
 
Naye mkuu wa kitengo wa kuthibiti dawa za kulevya nchini Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi(SACP) Mihayo Msikhela alisema Jeshi la Polisi nchini limejipanga hasa kwenye kuzuia kuliko kutibu ndio maana wameamua kuharibu mapema mimea ya zao hilo haramu kabla ya kukomaa na kusambaa.
 
Alisema kwamba kiwango cha uteketezaji wa dawa za kulevya hapa nchini kwa mwaka 2016 kiliongezeka ikilinganishwa na mwaka juzi 2015.
 
Kwa upande wake Afisa sheria mkuu toka Tume ya Kuratibu na Kuthibiti dawa za kulevya Bi. Christina Gervas alisema kwamba kadri bajeti itakaporuhusu watazidi kushirikiana na vyombo vya Usalama kufanya operesheni mara kwa mara katika maeneo ambayo bhangi inalimwa na pia kuahidi kutoa elimu kwa wakulima na viongozi wa maeneo hayo ili waweze kuachana na zao hilo haramu na kujikita kwenye mazao halali ya chakula na biashara.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa