KIU ya Mbunge wa Arusha Mjini, Gobless Lema kupata dhamana na
kujinasua kwenye mkono wa sheria baada ya kusota mahabusu kwa wiki nne
sasa, inazidi kufifia baada ya mawakili upande wa serikali kuwasilisha
pingamizi la rufaa ya mbunge huyo kusikilizwa katika Mahakama Kuu Kanda
ya Arusha.
Lema alishindwa kuingizwa katika chumba cha Mahakama kwa ajili ya
kusikiliza kesi yake, badala yake kwa muda wote tangu saa 2:14 asubuhi
hadi saa 6:18 mchana alikuwa mahabusu tu akisubiri kupelekwa mahakamani
na ndipo baada ya muda, alipanda basi dogo la Magereza kwenda Mahabusu
ya Kisongo ambako amekuwapo kwa zaidi ya siku 26 sasa kutokana na
kukwama kisheria kupata dhamana.
Rufaa hiyo imepingwa na mawakili wa Serikali ambao ni Paulo Kadushi
na Matereus Marandu wakidai kuwa rufaa iliyokatwa na mawakili wa Lema
haijakidhi matakwa ya kisheria kwa sababu mawakili hao walikata rufaa
badala ya kuonesha kusudio la kukata rufaa.
Materu alisema wamewasilisha pingamizi zao mbele ya Jaji Fatma
Masengi ya kupinga Mahakama Kuu kutosikiliza kesi ya dhamana kwa sababu
mawakili wanaomtetea Lema ambao ni Peter Kibatala na Sheck Mfinanga,
wamekosea kukata rufaa badala ya kuwasilisha notisi ya kusudio la kukata
rufaa ndani ya siku 10 baada ya awali Jaji kutupa ombi la kusikilizwa
kwa rufaa hiyo.
“Sisi leo tumeweka pingamizi la kusikilizwa kwa kesi hii sababu hawa
wenzetu wamekosea wao badala ya kuwasilisha pingamizi la kukata rufaa
wakakimbilia kukata rufaa na sheria haisemi hivyo lazima kwanza uoneshe
nia ya kukata rufaa ndipo ukate rufaa,” alieleza Materu.
Hivyo pingamizi la kusudio la kukata rufaa litawasilishwa kwa
maandishi kesho Novemba 30, mwaka huu saa 2:00 asubuhi, upande wa
serikali utawasilisha kwa maandishi hoja zao na saa sita mchana siku
hiyo hiyo, na upande wa mawakili wa Lema utajibu hoja za mawakili hao
kwa maandishi na Jaji, Masengi atapitia hoja hizo saa tisa alasiri.
Kisha Jaji Masengi atatoa uamuzi dhidi ya pingamizi hilo Desemba 2,
mwaka huu na endapo atakubaliana na upande wa serikali upande wa Lema
utakuwa umeshindwa na endapo hoja za Lema zikishinda dhidi ya pingamizi
la serikali, kesi ya msingi ya kusikilizwa kwa maombi ya dhamana ya
mbunge huyo itasikilizwa na kutolewa uamuzi.
Mawakili wa mbunge huyo wakiongozwa na Kibatala, walisema wao awali
walisajili maombi ya rufaa namba 112/113 ya mwaka 2016 Mahakama Kuu
Kanda ya Arusha ili kudai haki ya dhamana ya Lema aliyonyimwa kutokana
na makosa ya kisheria yaliyofanywa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment